Home SPORTS TUSIWATENGE WALA KUWANYANYAPAA WATOTO WENYE USONJI – MAJALIWA

TUSIWATENGE WALA KUWANYANYAPAA WATOTO WENYE USONJI – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii ya Watanzania kuacha kuwanyanyapaa watoto na watu wanaoishi na Usonji, magonjwa ya mfumo wa fahamu pamoja na matatizo ya akili.

Pia amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye changamoto za ukuaji au uelewa watafute ushauri kwa wataalam wa afya ili watoto wao waweze kufaidika na huduma zilizopo katika umri mdogo.

“Wataalam wetu muendelee kuongeza juhudi katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa haya ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na huduma.”

Ametoa wito huo leo ( Jumapili 28, Aprili 2024) alipokuwa akizungumza baada ya kushiriki mbio fupi za hisani za Run 4 Autism Tanzania, zilizofanyika katika viwanja vya The Green Ground Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

Kadhalika ameiagiza Wizara ya Afya kuongeza vituo vya huduma za uchunguzi hasa utambuzi wa mapema wa ugonjwa wa usonji na matatizo mengine ambayo yanaweza kubainika wakati watoto wanapoenda kwenye kliniki kila mwezi.

“Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI zihakikishe uwepo wa huduma jumuishi zinazoweza kuleta tija kwa kina mama na watoto ambao wanazaliwa na magonjwa ambayo yanaweza kubainika mapema.”

Aidha, ameitaka Wizara ya Elimu iendelee kongeza kasi ya upanuzi wa utoaji wa huduma za Elimu Jumuishi pamoja na kuongeza wigo wa mafunzo na vyumba vya madarasa katika shule nyingine ili watoto wenye ulemavu wasitembee umbali mrefu kwenda shule.

Pia amevitaka vyombo vya habari, wasanii na wanajamii kwa ujumla kutumia kila fursa kuielimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya.

“Wanahabari tumieni kalamu zenu kuelimisha jamii kuhusu afya na udhibiti wa magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya akili.”

Naye, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS), imeanzisha Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Mazoezi tiba ya kusaidia mawasiliano (Speech pathology), Tiba Kazi (Occupational therapy) na Tiba Viungo (Physiotherapy) na shahada ya kwanza ya Sayansi ya Saikolojia ya Kitabibu (Clinical Psychology) kuanza mwaka huu 2024.

“Lengo la kuanzishwa kwa shahada hizi ni kuhakikisha kuwa, huduma za utengemao zinapewa kipaumbele cha juu na Serikali.”

Awali, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Foundation ambao ndio waandaaji wa mbio hizo amesema lengo la mbio hizo ni kuchangisha fedha kiasi cha Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa miaka mitano kuanzia 2024 hadi 2028 wenye lengo la kukuza Ustawi wa Kila Mtoto mwenye viashiria vya usonji.

“Mkakati huu ni kwa ajili ya kuongezea nguvu mipango ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Afya kwa kuboresha uwezo wa walimu wa shule za Chekechea katika kubaini viashiria vya usonji kwa watoto.”

Ugonjwa wa Usonji kwa kiingereza Autism, ni ugonjwa ambao kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO hukumba mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 duniani.

Usonji ni tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea.

(mwisho)

Previous articleMATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA KISASA KUDHIBITI MAJANGA YA MIGODI YA BARRICK NCHINI YAPONGEZWA NA SERIKALI NA WANANCHI KATIKA MAONESHO YA OSHA
Next articleWAZIRI MKUU AFUNGUA SEMINA MAALUM KATIKA SEKTA YA KILIMO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here