Na: Saimon Mghendi, KAHAMA.
CHAMA kikuu cha Ushirika KACU kimesema kuwa kulingana na ubora wa Pamba inayochakatwa na kiwanda cha kuchambua Pamba kilichopo Kata ya Mhongolo wilayani Kahama Mkoani Shinyanga Ushirika huo umeanza kufanya biashara ya zao hilo na mataifa ya Ulaya jambo ambalo limesababisha zao hilo kuonekana kuwa na tija nchini.
Kaimu Meneja Mkuu wa chama hicho Abdul Ally amebainisha hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea kiwanda hicho.
Kaimu Meneja huyo amesema kuwa lengo la KACU kwa msimu huu wa zao la Pamba ni kununua kilo Milioni 6 kutoka kwa wakulima wa zao hilo wa halmashauri za Ushetu, Kahama, Msalala, Nyang’hwale, Kishapu na Meatu.
Kwa upande mwingine kiongozi huyo amesema kuwa chama chake cha ushirika kimejipanga kuanzisha kiwanda kingine cha kusindika mafuta ya kula ili kuongeza ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo na shinyanga kwa ujumla.
Hata hivyo kwa upande wao baadhi ya watumishi wa kiwanda hicho wamepongeza uongozi wa chama hicho cha ushirika kwa kuwapa vijana fursa za ajira wanaozagaa mitaani jambo linalopelekea kutunza familia zao na kuachana na vitendo viovu.
MWISHO.