Benki Kuu ya Congo (BCC) imeipatia leseni ya kufungua kampuni tanzu nchini humo Benki ya CRDB. Leseni hiyo imekabidhiwa leo katika mkutano maalum kati ya BCC na ujumbe wa Benki ya CRDB ulioongozwa na Afisa Mkuu wa Fedha wa Kundi, Fredrick Nshekanabo.
Akikabidhi leseni hiyo Naibu Gavana wa kwanza wa BCC, Dieudonné Fikiri Alimasi aliipongeza Benki ya CRDB kwa hatua hiyo muhimu ambapo alisema itakwenda kuchochea ushindani katika sekta ya fedha nchini humo kwa kutambua kuwa benki hiyo ni moja ya benki zinazofanya vizuri katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“Tulipopokea ombi lenu la kufungua kampuni tanzu hapa DRC tulifurahi na tulilichukulia kwa umuhimu mkubwa hasa ukizingatia mahusiano yaliyopo baina ya nchi zetu. Niwapongeze kwa namna ambavyo mlikuwa mkitoa ushirikiano katika kila ambalo tuliwaambia kutekeleza, hii inaonyesha jinsi gani mmedhamiria kuingia DRC na kufanya biashara hapa,” alisema Naibu Gavana BCC.
Katika taarifa yake kwa ujumbe wa Benki ya CRDB, Naibu Gavana pia alieleza kuwa BCC imepitisha mapendekezo ya uteuzi wa Bi. Jessica Nyachiro kama Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB nchini DRC.
BCC pia imewaidhinisha Dr. Fredrick Msemwa (Tanzania), Prof. Faustine Bee (Tanzania), Jeannot Okit’Otete (DRC), Olivier Duterme (DRC) Bi. Ornella Bomine (DRC), Bi. Rama Bweya (DRC) kuwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Congo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB aliishukuru BCC kwa kuipatia Benki hiyo leseni ya kufanya biashara nchini humo, na kueleza kuwa Benki ya CRDB imeshafanya maandalizi yote ya kufungua milango nchini humo. Nshekanabo alimuhakikishia Naibu Gavana kuwa Benki ya CRDB itashirikiana kwa karibu na BCC ili kusaidia kuimarisha sekta ya fedha nchini DRC.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Congo, Jessica Nyachiro amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatoa huduma bora na bunifu zitakazoendana na soko la DRC. Jessica alisema Benki ya CRDB itatumia uzoefu wake katika masoko ya Tanzania, na Burundi kuhakikisha ina kabiliana na ushindani nchini humo.
Akielezea mkakati wa kufikisha huduma kwa wateja, Jessica amesema Benki hiyo itaanza na tawi katika mji wa Lubumbashi, huku akieleza kuwa katika mkakati wake wa biashara wa miaka mitatu Benki ya CRDB Congo inatazamia kupanua wigo wake katika miji mengine mikubwa ikiwamo Kinshasa, Lualaba, Kasai, Kisangani, Tanganyika, pamoja na Kivu kaskazini na kusini.
“Benki yetu inasifika kwa uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali hivyo pamoja na mtandao wa matawi tunatarajia pia kutumia njia mbadala za ufikishaji huduma kama vile CRDB Wakala, SimBanking, na Internet banking kuwaunganisha wananchi wengi wa Congo katika huduma zetu,” amesema Jessica.
Jessica aliongezea kuwa malengo ya Benki ya CRDB ni kuwa mshirika namba moja wa maendeleo nchini DRC. Aliihakikishia Serikali na wadau wa sekta binafsi nchini humo kuwa Benki hiyo ipo tayari katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na sekta ya umma na binafsi.
“Benki yetu ina mizania kubwa ambayo inawezesha sekta zote za maendeleo. Kama ambavyo tumekuwa tukifanya Tanzania na Burundi huku pia tumejipanga kufanya hivyo,” huku akitoa mifano ya miradi ya Reli ya Kisasa (SGR) na ujenzi wa bandari ya Kigoma ambayo Benki hiyo inasaidia kuifadhili nchini Tanzania ambayo ikikamilika itasaidia pia nchi ya DRC.
Jessica aliwashukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Felix Tshisekedi Tshilombo kwa kazi nzuri ya kuboresha mahusiano baina ya Tanzania na DRC ambayo yamesaidia kurahisha Benki hiyo kupata kibali nchini humo.
Kwa upande wake Israel Tshimanga Mutamba, Afisa Mahusiano kwa Wateja wa Benki ya CRDB Congo aliwakaribisha wajasiriamali nchini humo hususan vijana na wanawake kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki hiyo huku akibainisha kuwa benki hiyo ina huduma mahsusi kwa ajili ya kundi hilo ikijumuisha mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa biashara na mikopo nafuu.
“Napenda kuwajulisha Wacongo wenzangu, hii ndio Benki ambayo tukiitumia vizuri tutaweza kuboresha maisha yetu. Uwe mwanafunzi, mfanyakazi, mkulima, mfanyabiashara, Benki ya CRDB ipo tayari kukuhudumia. Niwasihi tuchangamkie fursa hii,” aliongezea Israel.
Ujumbe wa Benki ya CRDB uliambatana na viongozi waandamizi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Congo wakiongozwa na Mkuu wa Utawala, Netho Yatega ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mchakato mzima wa kuhakikisha Benki ya CRDB inapata leseni ya kutoa huduma nchini humo.
Naibu Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Congo, Dieudonné Fikiri Alimasi (watatu kushoto) akikabidhi leseni ya kutoa huduma za kibenki nchini humo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Jessica Nyachiro. Wakishuhudia zoezi hilo ni Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (katikati), Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Congo, Netho Yatega (wapili kushoto), Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (watatu kulia), Mkurugenzi wa Hazina na Masoko ya Mitaji, Alex Ngusaru (wakwanza kulia), na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Benki ya CRDB, Yolanda Uriyo.
Naibu Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Congo, Dieudonné Fikiri Alimasi akiongoza kikao kabla ya kukaidhi leseni ya kutoa huduma za kibenki nchini Congo kwa uongozi wa Benki ya CRDB.