Home LOCAL WAKAZI WA NYASA WAJITOKEZA KWA WINGI KWENYE KAMPENI YA UCHUNGUZI WA KIFUA...

WAKAZI WA NYASA WAJITOKEZA KWA WINGI KWENYE KAMPENI YA UCHUNGUZI WA KIFUA KIKUU

Mkazi wa kijiji cha Kihagala wilayani Nyasa Yusta Kumburu(83 akisaidiwa na msamaria mwema Agnes Ndimbo kuteremka kwenye kliniki tembezi baada ya kupata vipimo vya ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni ya kupambana na ugonjwa huo iliyofanywa na wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Shirika la MDH-Amref Health Africa.

Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala,kitoa elimu ya ugonjwa wa kfua kikuu kwa wakazi wa kijiji cha Liuli wilayani Nyasa kabla ya kuanza kwa zoezi la uchunguzi wa ugonjwa huo.


Wakazi wa kijiji cha Liuli wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wakimsikiliza Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala(hayupo pichani)wakati wa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo.

 OLYMPUS DIGITAL CAMERA


Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Liuli wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wakiwa katika foleni kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni iliyofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo Shirika la MDH-Amrefu Health Africa katika vijiji vya Kihagala na Liuli wilayani Nyasa.

Picha zote na Muhidin Amri

Na: Muhidin Amri,Nyasa

JUMLA ya watu 110 kati ya 774 waliofanyiwa  uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kupitia kampeni ya kupambana na ugonjwa huo mkoani Ruvuma wamekutwa na maambukizi ya kifua kikuu.

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala alisema,kubainika kwa watu hao kunatokana na kampeni  kabambe ya kuwaibua  wagonjwa  wa kifua kikuu iliyofanywa  na  wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau shirika la MDH-Amref Health Africa.

Kwa mujibu wa Dkt Mbawala,kampeni hiyo imefanyika kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe 30 March hadi 12 April mkoani humo, ambapo wataalam  wa kitengo cha kifua kikuu walifanya kampeni katika maeneo ya migodi na vijiji vinavyozungukwa na machimbo ya madini.

Alisema, katika kampeni hiyo wilaya ya Tunduru ndiyo iliyoongoza kuwa na wagonjwa 87 ikifuatiwa na wilaya ya Mbinga wagonjwa 14 na wilaya mbili za Songea na Nyasa wameibuliwa wagonjwa 9.

Alisema, katika kampeni hiyo mwitikio wa wananchi ulikuwa mkubwa ndiyo maana katika kipindi kifupi wamefanikiwa kupata wagonjwa wengi na kuwataka wananchi wa mkoa Ruvuma kuwa na tabia ya kujitokeza kila kampeni zinapofanyika ili kufahamu hali ya afya zao.

Alisema, kwa mwaka 2022 mkoa wa Ruvuma umepewa lengo la kuibua wagonjwa 3,135 katika Halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma,na kueleza  kuwa wana uhakika wa kufika idadi hiyo na hata kuvuka lengo walilopewa.

Dkt Mbawala alisema,katika kampeni hiyo changamoto kubwa ilikuwa miundombinu mibovu ya barabara jambo lililochangia wataalam wa kitengo cha kifua kikuu kushindwa kufika kwa wananchi kwa wakati kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.

Aidha alisema,katika kampeni hiyo jumla ya watu 283 walipima virusi vya ukimwi na watu 9 walipatikana na virusi vya ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mratibu wa kifua kikuu wa wilaya ya Nyasa Dkt  Andrew Luwungo alisema, Halmashauri ya Nyasa kwa mwaka 2021 ilipewa lengo la kuibua wagonjwa 220 wa kifua kikuu,hata hivyo walifanikiwa kuibua jumla ya wagonjwa 310.

Alisema, wagonjwa wote waliweza kuunganishwa na matibabu ya kifua kikuu na hivyo kufanya wilaya hiyo kuvuka lengo kwa asilimia 140.9.

Dkt Andrew alieleza kuwa,kazi ya uibuaji wa wagonjwa wa kifua kikuu inatekelezwa na wataalam wa afya  na wahudumu wa afya ngazi ya jamii(CHW) ambao wana majukumu ya kupita mitaani kutafuta wagonjwa wa kifua kikuu,kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi.

Alitaja majukumu mengine ya wahudumu hao kuwa ni kutoa elimu ya ugonjwa wa kifua kikuu mitaani na kukusanya sampuli ya makohozi kwa wahisiwa na kuzifikisha kwenye maabara za vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha alisema,kwa mwaka 2022 wilaya hiyo kupitia kitengo cha kifua kikuu imepewa lengo la kuibua wagonjwa  300 na watafikia malengo hayo kwa kuwa wamejipanga  kufanya kazi  kwa bidii.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kihagala na Liuli Halmashauri ya wilaya Nyasa wameipongeza Serikali kupitia wizara ya Afya kwa jitihada inazofanya kuhakikisha wananchi wanafikishiwa huduma za uchunguzi wa ugonjwa huo katika maeneo yao.

Mkazi wa kijiji cha Kihagala Magreth Nombo alisema,kufikishiwa kwa huduma ya uchunguzi wa afya katika maeneo yao kutasaidia sana wananchi kutambua matatizo ya kiafya yanayowasumbua mapema na kuwa rahisi kukabiliana nayo kabla hali haijawa mbaya na kushauri utaratibu huo ufanyike mara kwa mara.

“Utaratibu huu unaofanywa na Serikali kupitia wizara ya afya  ni nzuri na utaokoa maisha ya watu wengi hasa wenye  hali duni ya maisha,tunaipongeza sana serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama Samia”alisema.

Aidha,ameipongeza Serikali kujenga kituo cha Afya Kihagala ambacho kimesaidia sana kusogeza na kutoa huduma bora za matibabu kwa wananchi hususani mama wajawazito na watoto.

Alisema,kabla ya kujengwa kwa kituo hicho wakazi wa kata ya Kihagala waliteseka kwa kusafiri umbali mrefu hadi kituo cha Afya Liuli na kituo cha Afya Mbambabay kufuata matibabu.

Mkazi wa kijiji cha Liuli Anna Kumburu ameomba kampeni hizo kufanyika mara kwa mara kwa kuwa zitawezesha wananchi kuwa na afya njema na hivyo kushiriki  kazi za maendeleo na kuondokana na umaskini katika familia zao.

Previous articleRAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA RAIS WA NATIONAL DEMOCRATIC INSTITUTE JIJINI WASHINGTON MAREKANI
Next articleKIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI KUTANGULIZA UZALENDO KATIKA MAJUKUMU YAO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here