Baadhi ya Washiriki wakifuatilia mafunzo ya BRELA. |
NJOMBE.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inatoa mafunzo kwa maafisa biashara kuhusu Sheria ya Leseni za Biashara pamoja na taratibu za utoaji wa leseni hizo. Mafunzo hayo yaliyoanza rasmi Juni 14, 2021 katika ukumbi wa Milimani Motel mkoani Njombe, yameshirikisha Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma
Afisa Leseni Mwandamizi kutoka BRELA Bw. Abas Cothema amesema lengo kuu la kuandaa mafunzo hayo ni kutoa elimu na hamasa kwa Maafisa Biashara ambao wamekuwa ni wadau wakubwa wa BRELA.
Amesema BRELA imejipanga kuwafikia Maafisa Biashara kote nchini na kuwapa elimu juu sheria za utoaji wa Leseni za Biashara, pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za sheria hiyo ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufasaha zaidi.
Bw.Cothema amesema mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni mojawapo ya mkakati wa BRELA wa kupunguza na hatimaye kuondoa tatizo la vishoka wanaokwamisha taratibu za upatikanaji wa Leseni kwa wafanyabishara.
Naye Afisa Biashara kutoka Mkoa wa Njombe Bw. Lusungu Essau Mbede licha ya kupongeza juhudi zinazofanywa na BRELA alieleza kuwa kumekuwa na changamoto kwa upande wa wafanyabiashara kwani baadhi yao hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu leseni na kushindwa kufuatilia kwa wakati leseni hizo.
“Nimefurahi kuwaona BRELA kwa kutukutanisha Maafisa Biashara wa Mikoa mitatu (Njombe, Iringa na Ruvuma) na kutupatia mafunzo haya muhimu”, alisema Bw. Lusungu Essau Mbede.
Mafunzo haya ya siku tano yanatarajia kuhitimishwa Juni 18, 2021.