WADAU wa usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani kupitia Bandari ya Dar es Salaam, wamekutana kujadili changamoto na fursa katika biashara ya kikanda, sambamba na kujengeana uelewa juu ya utekelezaji wa sheria na kanuni za ushindani wa haki.
Kikao hicho maalum kimehusisha taasisi mbalimbali zikiwemo TATOA, TPSF, Wizara ya Viwanda na Biashara, TPA, na Wizara ya Uchukuzi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio, amesema ushirikiano wa karibu baina ya sekta binafsi na taasisi za umma, ni muhimu kwa kuhakikisha kuwa bidhaa zinazopitia Bandari ya Dar es Salaam zinafuata viwango na sheria zilizowekwa, huku biashara zikiendeshwa kwa uwazi, ushindani wa haki, na bila usumbufu kwa wasafirishaji.
“Tumekutana kwaajili ya kujenga uelewa wa pamoja kuhakikisha kwamba kunakiwa na utekelezaji bora wa sheria, huku biashara zinakwenda vizuri bila kuleta malalamiko kutoka kwa wadau waliopo ndani na nje ya nchi kujua wana kero zipi na kukubaliana kwa pamoja namna ya kuzitatua. kwa lengo la kufanikisha biashara” amesema Erio
Amesema maeneo yaliyopewa kipaumbele ni udhibiti wa bidhaa bandia ambazo zinaathiri siyo tu afya na usalama wa walaji, bali pia ushindani wa haki kwa wafanyabiashara wa kweli, na kuongeza kuwa, jukumu la wadau hao ni kuhakikisha wanalilinda soko la ndani na kuimarisha taswira ya Tanzania kama kitovu cha biashara ya kikanda.
“Kampuni inayohusisha na usafirishaji wa bidhaa zinakusudiwa kupelekwa kwenye nchi jirani. Zilipofika nchini, FCC tulipata malalamiko kutoka kwa wamiliki wa nembo ya bidhaa ile kuwa bidhaa zinapofika kwenda nchi jirani ni zao na ni bandia na kwa mujibu wa sheria tunatakiwa tuzishughulikie” ameongeza Erio
Aidha, amesema lengo lao ni kujenga uelewa wa pamoja na kuhakikisha tatizo kama hilo halijitokezi tena na kuhakikisha wanafanyakazi kwa namna ambayo haitaleta malalamiko kama yaliyojitokeza.
Kwa ujumla, kikao hicho kimetoa mwanga kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na umma katika kukuza biashara ya kikanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam.