Home BUSINESS WAZIRI KAIRUKI AKUTANA NA WAANDAAJI WA ONESHO LA KUBWA LA UTALII DUNIANI...

WAZIRI KAIRUKI AKUTANA NA WAANDAAJI WA ONESHO LA KUBWA LA UTALII DUNIANI LA FITUR

Na: Mwandishi Wetu – Barcelona, Hispania

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Kampuni ya IFEMA ya Madrid, Hispania inayojihusisha na uandaaji wa Onesho linaloongoza duniani la Feria Internacional de Turismo (FITUR) lengo ikiwa ni kuangalia namna bora ya kuboresha ushiriki wa Tanzania katika Onesho hilo na kuitangaza zaidi Tanzania katika soko la Kimataifa.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Barcelona, Hispania leo Juni 10,2024 Waziri Kairuki amesema kuwa ushiriki wa Tanzania kwenye Onesho hilo utaifanya Tanzania kujulikana zaidi Kimataifa.

Aidha, amewahakikishia waandaaji hao kuwa Tanzania ina dhamira ya kuendelea kushiriki ipasavyo kwenye onesho hilo na iko tayari kupokea maoni na ushauri wa namna ya kuweza kuboresha zaidi ushiriki wake ili iweze kufanikiwa kujitangaza katika soko la Kimataifa hasa Hispania na Latin Amerika.

Mwaka 2023 Hispania ilishika nafasi ya pili kwa kuwa eneo linalotembelewa zaidi duniani kwa kuingiza watalii wa kimataifa milioni 85, ikifuatiwa na Marekani (watalii milioni 66), Italia (watalii milioni 57) na Türkiye, ambayo ilifunga tano bora kwa kuwa na watalii milioni 55 wa kimataifa.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IFEMA, Bi. María Valcarce amesema kuwa onesho la FITUR ni soko kubwa la kimataifa la utalii linalopata washiriki takribani 152,000 ambao ni waendesha watalii, mashirika mbalimbali na wageni takribani 92,000.

Aidha, amesema IFEMA iko tayari kushirikiana na Tanzania kuangalia namna bora ya kufanikisha ushiriki wake katika maonesho yajayo.

“Tunataka kuitangaza Afrika kupitia FITUR na kuwaleta watu wa Hispania kuijua Afrika na mnyororo mzima wa biashara katika sekta ya utalii” amesisitiza Valcarce.

Waziri Kairuki yupo jijini Barcelona Hispania kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa 121 wa Baraza Tendaji la Shirika la Utalii Duniani utakaofanyika kesho Juni 11, 2024 jijini Barcelona, Hispania.

Previous articleWAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI TPDC WAFANYA ZIARA GASCO
Next articleNAULI MPYA ZA ABIRIA KWA DARAJA LA KAWAIDA – TRENI YA KISASA (SGR)
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here