Afisa Mwandamizi Mkuu Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu BoT Bi.Crispina Nkya akizungumza na waandishi wa habari katika banda la benki hiyo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo NaneNane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Catherine Katanana Afisa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu BoT akitoa maelezo kuhusu utunzaji wa noti na sarafu kwa wananchi waliotembelea katika banda la benki hiyo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo NaneNane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Neema Hashim Afisa Kutoka Kurugenzi ya Huduma za Kibenki BoT akitoa maelezo kwa mmoja wa wananchi waliotembelea katika banda hilo.
Na: John Bukuku, MBEYA
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa Rai Kwa wananchi Kutunza Fedha zao katika sehemu safi na salama ili kuepuka uchakavu wa Fedha hizo.
Akizungumza kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Afisa Mwandamizi Mkuu Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu BoT Bi.Crispina Nkya amesema serikali inatumia pesa nyingi kuchapisha fedha mpya hivyo ni jukumu la Kila mwananchi kutunza Pesa zake zisichakae Wala kuchanika.
“Sisi tuna sera inayoitwa Sera ya Fedha Safi lengo lake ni kuhakikisha kwamba noti zinazotumika zipo kwenye Hali nzuri Kwa ajili ya watumiaji na kuziondoa kwenye mzunguko zile Fedha zote ambazo ni chakavu” amesema Nkya
Aidha Nkya ameongeza kuwa katika mzunguko wa Fedha sera hiyo inasisitiza ujazo wa Fedha kwenye mzunguko na katika sehemu kubwa ya uchumi ambapo katika mzunguko wa Fedha imeweka ujazo wa Hela zote ikiwemo noti na sarafu.
Amesema sera inataka kila mwananchi kutunza fedha hizo ili kuisaidia serikali kupunguza gharama za matumizi ya kuchapisha fedha hizo kwani serikali inatumia fedha za kigeni kuchapisha Fedha nje ya nchi.
“Tunapenda wananchi watunze Fedha sehemu salama na si kuziweka kwenye mikunjo ya Khanga.kuzichimbia chini,kuzitoboa,kuweka kwenye Soksi,kwenye Magoforo au kwenye Nguo za ndani kwa kufanya hivyo unaharibu fedha.”
Aidha Nkya amesisitiza kuwa noti na sarafu zihifadhiwe sehemu salama ili kukwepa kujikunjakunja na kuchanika Hali inayopelekea uchakavu wa noti hizo.
Banki kuu ya Tanzania kupitia Kurugenzi ya Sarafu ndio inayohusika kuchapisha Fedha Mpya na kuziondoa Fedha chakavu kwenye mzunguko na kuzihifadhi.