Home LOCAL MAJALIWA AAGIZA JIJI LA DODOMA, LATRA KUKUTANA

MAJALIWA AAGIZA JIJI LA DODOMA, LATRA KUKUTANA

*Ni kushughulikia mpango wa stendi katika soko jipya la wajasiriamali Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jiji la Dodoma ukutane na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) ili kutengeneza mpangilio safari za daladala ndani ya jiji hilo kuelekea soko jipya la wajasiriamali wadogo lililoko barabara ya Bahi.

Amesema sambamba na utekelezaji wa maagizo hayo Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanafanya maboresho ya stendi iliyoko katika eneo hilo ili iweze kukidhi viwango vya kupokea magari ya abiria yatakayoelekezwa eneo hilo.

Ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi Novemba 24, 2022) mara baada ya kukagua soko jipya la wajasiriamali wadogo lililoko Bahi Road jijini Dodoma.

Pia ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma isimamie utoaji wa fedha za mikopo kwa wafanyabiashara katika soko hilo ili waongeze mitaji na kukuza biashara zao.

“Nataka nipongeze uamuzi wenu wa kuja hapa mmefanya maamuzi sahihi na mtanufaika.”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ni dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuwainua wafanyabiashara kwa kufungua milango ya ufanyaji biashara kwa uwazi na Serikali kuwapa huduma muhimu zitakazowasaidia kuleta tija kwenye shughuli zao.

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha anafanyia kazi changamoto zilizojitokeza baada ya wafanyabiashara kuhamia katika eneo hilo ikiwemo kuboresha barabara, vikingia mvua, taa za barabarani pamoja na kushirikiana na TARURA kuweka taa za barabarani.

Awali akijibu maombi ya wafanyabiashara hao, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema Halmashauri ya Jiji imetenga Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kutoa mikopo midogo kwa wafanyabiashara walioko na hadi kufikia mwezi disemba mwaka huu watakuwa wameshakamilisha taratibu za utoaji wa mikopo hiyo.

Naye Naibu waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Festo Dugange amesema ujenzi wa soko hilo ni dhamira njema ya Rais Samia Sulluhu Hassan ya kuwajali na kuwapenda wafanyabiashara wadogo wadogo waondokane na adha ya kutembea na bidhaa zao badala yake wapate sehemu nzuri na bora ya kufanya biashara zao.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wadogo Mkoa wa Dodoma Bw. Chrisrian Mohamed Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za kujenga soko hilo ambalo litafungua fursa kwa wajasiriamali hao.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S.L. P. 980,

41193 – DODOMA

ALHAMISI, NOVEMBA 24, 2022.

Previous articleDKT.MPANGO: BoT HAKIKISHA TAASISI ZA FEDHA ZINAPUNGUZA RIBA
Next articleWAZIRI KIJAJI AZISHAURI NCHI ZA AFRIKA KUTUMIA KISWAHILI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here