Baadhi ya wanahabari wakiuliza maswali anuai kwenye warsha hiyo |
Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Joyce Makwata (kulia) akifafanua jambo kwa wanahabari kwenye semina hiyo.
Na: Mwandishi Wetu, Kibaha
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewapongeza wanahabari kwa kuendelea kuijuza jamii juu ya taarifa mbalimbali za mabadiliko ya hali ya hewa nchini zinazotolewa na mamlaka hiyo.
Kauli hiyoimetolewa leo Mjini Kibaha na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a alipozungumza akifungua warsha ya wanahabari iliyoandaliwa na TMA ili kuendelea kuwajengea uwezo wanahabari juu ya kuripoti vizuri habari za hali ya hewa.
Alisema TMA inatambua kazi nzuri inayofanywa na wanahabari kupitia vyombo vyao vya habari kwani imeongeza mwamko wa jamii kufuatilia taarifa hizo.
“Ni kipindi kirefu sasa tangu tumeanza kuwa na warsha kama hizi kwenu wanahabari mara kwa mara kila tunapokaribia kutoa utabiri wa msimu. Kwa hakika matokeo tumeyaona kwani kwa msaada wenu tumeona mwamko na uelewa wa jamii juu ya Taarifa za hali ya hewa kuongezeka,” alisema Dk. Chang’a.
Aidha alieleza kuwa TMA itaendelea kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari ili kuhakikisha kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa kwa uhakika, usahihi na kwa wakati.
Alisema lengo la warsha hiyo ni kuwaandaa wanahabari kupokea taarifa ya mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2021, ikiwa na kauli mbiu ya “Zingatia Tahadhari Kujenga Ustahimilivu”.
Alibainisha kuwa kuongezeka kwa mwamko na uelewa kuhusu taarifa za hali ya hewa kwa jamii zinapoifikia kwa uhakika ni muhimu kwani inasaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa zinapojitokeza.
“Hivyo, taarifa sahihi za hali ya hewa ni muhimu kupatikana kwa wakati pamoja na athari zake ili kuweza kujipanga na kujiandaa katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.“ Alisema.
Credit – Fullshangwe Blog.
Credit – Fullshangwe Blog.