Home SPORTS CLOCK TOWER MARATHON YAZINDULIWA RASMI JIJINI ARUSHA SASA KUTIMUA VUMBI...

CLOCK TOWER MARATHON YAZINDULIWA RASMI JIJINI ARUSHA SASA KUTIMUA VUMBI AGOSTI 8 MWAKA HUU, MEYA ASEMA YATAFUFUA UTALII.

 

Waandaji wa mbio za Clock Tower Marathon  Arusha Runners wakiwa katika picha ya pamoja na Meya wa jiji la Arusha Maxmilan Iranghe katika picha ya pamoja iliyopigwa katika eneo ambalo ndio katikati ya bara la Afrika mahali ambapo ndiopo mbio hizo zitakapoanzia.

Meya wa jiji la Arusha Maxmilan Iranghe (katikati) Akizungumza wakati wa uzinduzi huo.  Kulia kwake ni  Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Tanzania  John Bayona, na (kushoto) ni mwenyekiti wa clabu ya Arusha runners Isack Shayo.

Mwenyekiti wa clabu ya Arusha runners ambao ni waandaji wa mbio hizo Isack Shayo akiongea na waandishi wa habari baada ya uzinduzi rasmi wa mbio hizo.

NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.

Mbio za Clock Tower zinazoandaliwa na clabu ya  Arusha runners zimezinduliwa rasmi na zinatarajiwa kufanyika August 8 kwa mbio za kilometa 21, kilometa 10 pamoja na kilometa 5.

Akizindua mbio hizo Meya wa jiji la Arusha Maxmilan Iranghe alisema kuwa mbio hizo zitafufua utalii katika jiji hilo kutokana  na  zinafanyika katikati ya bara la Afrika ambapo pia aliwataka waandaji kuhakikisha mbio hizo zinafanyika kila mwaka.

“Kupitia mbio hizi mtalitangaza jiji la Arusha na naamini kwamba hamjawa na muaamko wa kuanzisha mkashindwa kumalizia, tunataka yawe endelevu na kila mwaka wakazi wa Arusha, mikoa ya jirani na watalii waweze kushiriki katika mbio hizi,” Alisema Meya Maxmilan.

Alisema kuwa jiji la Arusha limejipanga kuhakikisha mbio hizo zinafanikiwa kwani zina manufaa makubwa kwa wananchi na serikali kwa ujumla ambapo aliwataka wananchi kutoka maeneo mbalimbali kujiandikisha katika ushiriki ili kushindana pamoja na  kuweza kuzijenga afya zao na kulitangaza taifa kwa mbio hizo kuanza katikati ya bara la Afrika.

Kwa upande wake Isack Shayo mwenyekiti clabu ya Arusha runners alisema kuwa mbio hizo zitakazoanzia katikati ya bara la Afrika(CLOCK TOWER)  na kumalizikia katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid zitakuwa na mbio za kilometa 21, 10, na 5 ambazo  zote kwa pamoja gharama ya usajili ni shilingi 35000.

Shayo alieleza kuwa lengo la mbio hizo kuchangia damu kwa wahitaji na hasa kipindi hiki ambapo hamasa ya uchangiaji damu umekuwa mdogo katika taifa jambo ambalo wanaamini wataweza kuchangisha kiasi kikubwa cha damu na kuweza kuokoa maisha.

“Pamoja na uchangiaji wa damu lakini pia clabu yetu kila mwisho wa mwaka tumekuwa na utaratibu wa kuwasaidia wahitaji hivyo pia pesa zitakazo patikana zitatumika kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali, Alieleza Shayo.

Naye Katibu wa chama Cha riadha mkoa wa Arusha Rogath Steven alisema kuwa mbio hizo zitakuwa sehemu ya kuinua riadha hapa nchini na kama chama ndani ya mkoa wanaunga mkono kwani wanatambua mchango wake ambapo pia aliwataka wadau wengine wa riadha kufanya mbio zao mkoa wa Arusha kwani barabara ni nzuri, hali ya hewa pamoja na usalama .

“Kwa mbio hizi zinazotarajiwa kufanyika August 8 watu wasiwe na wasiwasi kwani zitasimamiwa kitaalamu na hakutakuwa na malalamiko kutoka na waandaji kuwa  wataalamu wa riadha  hivyo niwaombe watanzania kujiandikisha kwa wingi kwani kwa mwaka huu Arusha hakuna mbio nzuri kama hii,”Alisema.

Pia makamu mwenyekiti wa chama Cha riadha Tanzania John Bayo alisema kuwa riadha ina mitazamo miwili ambayo  kuibua vipaji na kutangaza riadha  pamoja na kurekebisha au kulinda afya hivyo wahakikishe mbio hizo zinakuwa mbio za heshima katika mji wa Arusha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here