Baadhi ya watumishi wa STAMICO walioshiriki maandamano ya Mei Meo katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam mara baada ya kupita mbele ya Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa Amos Makalla (hayumo pichani) PICHA NA: HUGHES DUGILO.
Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM.
Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo Mei 01, 2022 wameungana na Wafanyakazi wengine Duniani kote kusherehekea sikukuu ya Wafanyakazi Duniani kwa kushiriki maandamano katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam na Kiwira -Songwe
Akiongea kuhusu maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema, STAMICO imeshiriki katika kuadhimisha siku hii ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango unaofanywa na Wafanyakazi wa Shirika hilo katika kuhakikisha miradi yake inaendelea kwa ufanisi.
Amesema siku hii ni muhimu na inaleta hamasa miongoni wa wafanyakazi kwa kuwa kuna baadhi ya watumishi hao wameibuka kuwa Wafanyakazi hodari katika idara zao hivyo kuwa chachu kwa wengine kufanyakazi kwa bidii na ufanisi.
Amewataka wafanyakazi wote kushikamana katika kufanya kazi na kuongeza bidii ili kuleta tija kwa Shirika na miradi yake.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Deusdedith Magala amesema STAMICO inaendelea kuthamini mchango wa Wafanyakazi wake katika kuleta ubunifu na uthubutu jambo lililopelekea Shirika kufanikiwa sambamba na kuzalisha bidhaa mpya ya Mkaa mbadala wa kupikia ujulikanao kwa jina la Rafiki Briquette.
Amesema jitihada hizi zina maana kubwa katika kuleta ufanisi wa Shirika na hivyo wanastahili kupongezwa
Kwa upande wa Wafanyakazi, Bw. Samwel Kibaranga ambaye ameibuka kuwa mfanyakazi Hodari wa Shirika ameishukuru STAMICO kwa kutambua mchango wa kazi wanazozifanya na kutoa zawadi ya Wafanyakazi Hodari na kwamba nafasi hiyo ameichukua kama chachu kwa kuongeza juhudi na boresha utendaji kazi wake katika kipindi kijacho.
Amesema siri kuu ya ushindi wake ni kuwa na nidhamu, uthubutu, kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika kutekeleza majukumu yake.
STAMICO imeendelea kuungana na Taasisi nyingine za Serikali kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo kitaifa yamefanyika jijini Dodoma, Mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.