Na: Mwandishi Wetu.
MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo ametoa maelekezo kuhusu Stendi ya mabasi yanayofanya safari zake kuelekea mikoa ya kusini ambayo imehamia rasmi eneo la Kijichi na safari zote kuanzia leo Oktoba 17 zitaanza na kuishia hapo.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi stendi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo amewataka wakazi wa eneo na wafanyabiashara walio katika eneo hilo kuitumia vyema fursa ya kuanza kwa stendi hiyo.
Jokate ambaye alianza kwa kukagua njia yatakapopita magari kuelekea kwenye eneo hilo la stendi amesema Serikali imetimiza wajibu wake kujenga miundombinu ni jukumu la wananchi kuitumia na kuitunza stendi hiyo.
Amewataka wakazi wa eneo hilo kushirikiana na Jeshi la polisi kuhakikisha stendi hiyo inakuwa salama wakati wote na watu wanaingia na kutoka bila kuwa na wasiwasi wa usalama wao.
“Huku Kijichi kuna sifa ya matukio ya uhalifu sasa niwatake polisi mhakikishe ulinzi unaimarishwa wakati wote kwa ajili ya kulinda watu na mali zao.Wananchi pia suala hili msiliache kwa polisi pekee, ulinzi ni jukumu letu sote na iwe ajenda yetu ya kudumu maana eneo limeshakuwa na stendi kubwa hatutaki sifa kwamba stendi ya Temeke ina wizi,”amesema Jokate.
Kwa upande wake Raymond Samson akizungumza kwa niaba ya Chama cha wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) amepongeza hatua hiyo ya manispaa kutengeneza stendi ambayo sasa ndiyo itatambuloka rasmi kwa magari ya kusini.
“Tunapongeza hatua hii ila tunaomba changamoto ndogo ndogo ambazo zimeonekana zifanyiwe kazi kwa haraka ili ziondoe vikwazo kwa madereva kuleta magari huku,” amesema Samson.