Ripoti ya Said Mwishehe Msagala (MICHUZI BLOG).
HATIMAYE Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, imetoa maelekezo kwa Serikali kuona umuhimu wa kusikiliza maoni na ushauri wa wananchi kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Serikali hususani katika eneo la Tozo za miamala ya kielektroniki, iliyoanza kutekelezwa hivi karibuni.
Akizungumza leo Septemba 8,2022 wakati akitoa taarifa ya kikao NEC,Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Shaka Hamdu Shaka amesema pamoja na mambo mengine Kamati Kuu imepokea na kutafakari kuhusu hatua za kibajeti zinazoendelea kuchukuliwa kwa lengo la kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi.
“Eneo moja wapo ikiwa ni kupitia tozo ambapo ni ukweli usiopingika Serikali imefanya mambo makubwa katika kipindi kifupi kwa mfano ujenzi wa vituo vya afya 234, shule mpya za sekondari 214 na maeneo mengine kadhaa yanayogusa maisha ya Watanzania ya kila siku.
“Baada ya kutafakari na kujadiliana kwa kina Kamati Kuu imeona umuhimu wa serikali kusikiliza maoni na ushauri wa wananchi kuhusu utekelezaji wa bajeti hiyo, hususani katika eneo la tozo za miamala ya kielektroniki iliyoanza kutekelezwa hivi karibuni.
“Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imeielekeza Serikali kutazama hali halisi na kuchukua hatua stahiki kuhusu ushauri na maoni hayo ya wananchi kuhusu tozo hizo,” amesema na kufafanua
maelekezo hayo yamezingatia ibara ya 20(b) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.
Ameeleza Ilani inasema hivi “Kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa gharama nafuu kwa kupanua wigo wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za kifedha ili kuongeza huduma jumuishi za fedha nchini, kuchochea uwekezaji wa ndani na kukidhi mahitaji halisi ya wananchi hususan wa kipato cha chini na waishio vijijini.”
Aidha amesema Kamati Kuu ya CCM imeelekeza Serikali kufikiria na kujielekeza kubana matumizi, kujenga mazingira rafiki na wezeshi ili kujenga uchumi imara unaozalisha kwa lengo la kutanua wigo wa kodi pamoja na kubuni vyanzo vipya vya kodi ili kuwa na viwango pamoja na mfumo rafiki wa kodi kwa kila