Serikali ya Tanzania na Serikali ya Venezuella zimesaini Hati za Makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kisiasa na mkataba wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali baina ya nchi hizo.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
“Tumesaini mikataba miwili ambapo mmoja unalenga kuendeleza majadiliano ya kisiasa (political consultation) lakini pia makubaliano ya kuwa na ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kichumi, nishati, afya, elimu na kilimo,” amesema Balozi Mulamula.
Kusainiwa kwa mikataba hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Tanzania na Venezuela katika sekta za nishati, afya, elimu na kilimo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo miwili ni hatua muhimu ya kudumisha na kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali baina ya Venezuela na Tanzania.
Mhe. Moura amewasili nchini leo akitokea Venezuela na yupo nchini kwa siku mbili kwa ziara ya kikazi.