Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 Bi. Anne Makinda (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24,2022 Jijini Dar es Salaam kuhusu Maendeleo ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 Bi. Anne Makinda akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24,2022 Jijini Dar es Salaam kuhusu Maendeleo ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi
(PICHA NA: EMMANUEL MBATILO)
Na: Grace Semfuko, MAELEZO, Agosti 24, 2022
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 Bi. Anne Makinda amesema, zoezi la Sensa limeanza vyema na linaendelea vizuri kama ilivyopangwa ambapo hadi kufikia asubuhi ya Agosti 24, 2022, taarifa zinaonesha kuwa asilimia 17.13 ya kaya zilizopo nchini ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 15.0 lililokadiriwa kukamilishwa kwa siku ya kwanza zimehesabiwa.
Amesema taarifa hizo ni kwa mujibu wa mfumo wa ufuatiliaji wa ukusanyaji wa taarifa ambapo kituo cha kuchakata taarifa za Sensa kipo Jijini Dodoma
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu Maendeleo ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi,Bi Makinda amesema zoezi hilo litaendelea kwa siku saba kwa kurejea taarifa za Agosti 23 kama ilivvyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipozungumza na Watanzania mara baada ya kuhesabiwa.
“Kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan jana mara baada ya kuhesabiwa, alisema sio watu wote wangeweza kuhesabiwa jana tarehe 23 Agosti, 2022 pekee, ndio maana zoezi hili limepangwa kufanyika kwa siku saba, tnafahamu kuwa kila mwananchi angependa kuhesabiwa jana tarehe 23 Agosti, 2022 ambapo ilikuwa ni siku ya mapumziko akiwa katika kaya yake lakini ilikuwa sio rahisi. Hivyo tunawaomba wananchi wa kaya zote ambazo bado Karani wa Sensa hajafika kuwahesabu wawe na subira Karani wa Sensa atafika ndani ya siku sita zilizobaki” Amesema Bi Makinda.
Amesema ingawa zoezi hilo ni la siku saba, lakini taarifa za wanakaya zinazohitajika ni za watu wote ambao walilala katika kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa, yaani tarehe 22 Agosti kuamkia tarehe 23 Agosti, 2022 na kuwataka wakazi kuacha taarifa zao nyumbani ikiwepo kujaza fomu maalum ambayo Mkuu wa Kaya atajaza taarifa muhimu za watu wote waliolala katika kaya yake usiku wa kuamkia siku ya Sensa.
Aidha,kuhusu suala la viongozi wa mitaa na vitongoji kuongozana na makarani wa Sensa, Bi Makinda amesisitiza kuwa, kila kiongozi mmoja anapaswa kumuongoza karani mmoja wa Sensa, na malipo yao yameandaliwa huku akitolea mfano uzoefu walioupata Agosti 23, 2022 kuwa ni baadhi ya viongozi hao wanalazimisha kuongoza makarani zaidi ya mmoja jambo ambalo linachelewesha zoezi la Sensa.
Katika hatua nyingine Bi. Makinda amesema kumejitokeza changamoto za mipaka wakati wa kuhesabu watu na kuongeza kuwa Sensa ya Watu na Makazi haina mamlaka ya kurekebisha mipaka na kwamba zoezi la Sensa linatumia maeneo ya kuhesabia watu yaliyotengwa maalum kwa kazi hiyo.