KIKOSI cha Simba leo wametumia mchezo wao dhdi ya KMC kumuaga mchezaji wao Rally Bwalya ushindi wa mabao 3-1.
Hata hivyo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa na nje ya kuwa mechi ya ligi lakini Simba imeitumia kumuaga kiungo wake huyo iliyemuuza Amazulu FC ya Afrika Kusini.
Katika mchezo huo, timu zote zilianza kucheza kwa utulivu huku pasi fupi fupi zikipigwa kwa pande zote mbili.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba ikiwa nyuma kwa bao 1-0, lililofungwa na winga wa KMC, Hassan Kabunda dakika ya 41.
Kipindi cha pili kilirejea kwa Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa kiungo mkabaji Sadio Kanoute na kuingia mshambuliaji Peter Banda.
Ingizo la Banda lilionekana kuzaa matunda na kuifanya Simba kuongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa KMC.
Dakika ya 51 Simba ilipata bao la kusawazisha lililofungwa na Kibu Denis akimalizia krosi ya Pape Sakho.
Baada ya bao hilo, KMC ilifanya mabadiliko ya wachezaji wawili kwa kuingia Kenny Ally na Abdul Hilaly waliochukua nafasi za Awesu Awesu na Miraji Athuman.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuisaidia KMC kwani dakika ya 62 Simba ilipata bao la uongozi likifungwa na Sakho.
Pia katika dakika tatu Simba ilipata bao la tatu kupitia kwa Henoc Inonga akifunga kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Sakho.
Baada ya bao hilo Simba iliendelea kutafuta bao la nne lakini umakini kwenye eneo la mwisho ulipungua na matokeo kusalia hivyo hadi dakika ya 90.
Kibu, Sakho na Erasto Nyoni walifanyiwa mabadiliko na nafasi zao kuchukuliwa na Meddie Kagere, Taddeo Lwanga na Jimmyson Mwanuke.
Dakika ya 86, Simba ilimtoa Bwalya na kuingia Yusuph Mhilu ambaye hakubadili matokeo na mechi kumalizika kwa Simba kushinda 3-1.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha alama 57 katika nafasi ya pili kwenye msimamo huku KMC ikibaki na pointi zake 32 nafasi ya 10.