Home BUSINESS WAFANYABIASHARA MARA WAOMBA KUPUNGUZIWA UTITIRI WA TOZO

WAFANYABIASHARA MARA WAOMBA KUPUNGUZIWA UTITIRI WA TOZO

MARA.

WAFANYABIASHARA kutoka halmashauri zote katika Mkoa wa Mara, wamekutana kwenye jukwaa la wadau wa kodi na kueleza changamoto wanazokabiliana nazo katika kulipa kodi ikiwamo wingi wa tozo na kuomba serikali ione uwezekano wa kuzipunguza.

Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoani humo, Boniphace Ndengo alisema hayo kwenye mkutano huo uliyohusisha watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi, mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Chochote kinachotozwa na kupelekwa serikalini, kama siyo gharama za huduma za uendeshaji mfanyabiashara anakiita kodi, zinapokuwa nyingi zinachochea kukwepa kuzilipa,” alisema Ndengo.

Kwa mujibu wa utafiti wake usiyo rasmi, alisema mfanyabiashara mwaminifu akilipa kodi zote kama inavyotakiwa, kwa mwaka atalipa kati ya asilimia 70 mpaka 90 ya mapato yake na njia rahisi ya kumfanya abakize kipato zaidi, ni kukwepa kulipa kodi.

Alisema tozo zipunguzwe na mtaji wa kila biashara inayotozwa kodi usajiliwe, huku wajibu wa kuulinda mtaji na kuukuza uwe wa serikali ili wanaotoza kodi, waache kula mpaka mtaji.

Utaratibu wa taarifa za benki za wafanyabiashara kutumiwa na maofisa wa TRA, kupata uhalisia wa kujijengea misingi ya kukusanya kodi, utaratibu ambao unatafsiriwa kuwa ni kutozwa kodi isivyo halali inayosababisha baadhi ya wafanyabiashara kuacha kutunza fedha benki.

Alisema mapato ya wafanyabiashara hao yamekuwa yakifichwa na hivyo serikali kukosa mapato, shughuli za benki kuathiriwa na bila shaka mfumo mzima wa uchumi wa nchi kudorora.

Meneja Msaidizi Madeni wa TRA mkoani humo, Nuhu Msangi alisema hoja ya wingi wa tozo waliipokea na itafanyiwa kazi.

Kuhusu matumizi ya taarifa za kibenki katika kudai kodi alisema utaratibu huo upo kisheria na hutumiwa kwa mtu mjeuri, anayedaiwa deni halali, lakini asiyetaka kulipa ilhali ana pesa benki.

Alisema hata Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alishasisitiza kuwa hataki matumizi mabaya ya utaratibu huo na kwamba TRA hutumia njia hiyo baada ya njia nyingine za kumshawishi kulipa kushindikana na lazima kuwe na ushahidi unaothibitisha wamekutana naye si chini ya mara Tano.

Mwisho.

Previous articleSUA YAWAJENGEA UWEZO MAFUNDI SANIFU NCHINI KUHAKIKISHA UBORA WA BIDHAA ZA MIMEA DAWA
Next articleSERIKALI KUHAKIKISHA HUDUMA ZA VIPIMO VYA SIKOSELI ZINAPATIKANA KATIKA VITUO VYA AFYA NCHINI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here