Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC, Ahmed Abdallah Ahmed, akizungumza na waandishi wa Habari (Wamo pichani), mara baada ya kutembelea Banda la Shirika hilo kwenye maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC, Ahmed Abdallah Ahmed, (kushoto), akipokelewa na Meneja Uhusiano na Habari wa Shirika hilo, Muungano Saguya (kulia), mara baada ya kuwasili kwenye Banda lao.
(Picha na: HUGHES DUGILO)
Na Hughes Dugilo, DAR ES SALAAMÂ
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Ahmed Abdallah Ahmed, amesema kuwa Shirika hilo linaendelea kutekeleza mikakati iiyojiwekea kwa kukamilisha miradi yake kwa wakati.
Ahmed amebainisha hayo alipozungumza na waandishi wa Habari wakati alipotembelea Banda la Shirika hilo kwenye maonesho ya 48 ya Kibiashara ya Kimataifa (Sabasaba), yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Amesema, maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kupata taarifa mbalimbali za Shirika hilo na kufamu miradi wanayoitekeleza ikiwemo miradi mikubwa mitatu ya Jijini Dar es Salaam, ya Samia Housing Scheme, Kawe 77, na Morocco Square ambayo ipo katika hatua nzuri na mingine kukamilika.
Aidha, ameongeza kuwa katika Maonesho ya mwaka huu wanatoa huduma maalum kwa wananchi na wadau wanaotaka miradi ya ubia na kutoa taarifa mbalimbali kuhusiana na miradi hiyo.
“Wiki moja iliyopita tumetangaza miradi ya ubia katika maeneo mbalimbali nchini na hapa Sabasaba tumeweka dirisha maalum ili kutoa fursa kwa wananchi na wadau wanaotaka kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na miradi yetu ya ubia” amesema Ahmed.
Aidha ameeleza kuwa wameweka dawati kwaajili ya nyumba za kupangisha ambapo amefafanua kuwa mpangaji atapata taarifa kuhusiana na nyumba hizo na kuweza kupata nyumba kwakufuata taratibu.
Amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwawezesha kama shirika kuwaruhusu kuendelea kuchuka mikopo katika taasisi za kifedha.
Vilevile Ahmed ameeleza mikakati ya Shirika hilo la kuwafikia wananchi wa kipato cha kati na chini, nakusema kuwa wanaendelea kutekeleza kwa vitendo, nakwamba hawajawatupa mkono.
“Ukiangalia Mradi wa Samia Housing Scheme utaona nyumba 560 lakini tuliowakusudia pale ni Watanzania wa kima cha chini.
“Pale tuna nyumba ya chini ya million 50 na Bahati nzuri Serikali yetu imetoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), katika nyumba yenye thamani chini ya milioni 50” ameeleza Ahmed.
Ameongeza kuwa nyumba hizo sasa zimekuwa kimbilio la Watanzania wengi kwani wanazikimbilia.