MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa kwa sasa kuna vitaru zaidi ya 20 nchi kavu na vingine zaidi ya 14 Baharini ambavyo wanapanga kuvitangaza kwaajili ya kupata wawekezaji katika kipindi cha mwisho wa mwaka ujao na kwamba kwa sasa wanaandaa mkataba kifani (Model PSA) unaoendana na mazingira ya sasa kiuchumi, kimazingira na hali ya mafuta Duniani.
Mhandisi Sangweni ameyasema hayo leo Julai 7,2022 alipokuwa kwenye mahojiano na waandishi wa habari kwenye Maonsho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kwa sasa mchakato huo upo katika hatua nzuri na kwamba tayari mshauri mwelekezi amepatikana ambaye anasaidia kuuandaa na baadae watakwenda sokoni ili kuvitangaza rasmi na kupata mwekezaji kwaajili ya utafutaji wa Mafuta na Gesi.
“Kwasasa hivi Dunia inatoka kwenye matumizi ya Nishati inayochafua mazingira na tunaenda kwenye nishati jadidifu ambayo tunaamini ni Nishati safi na salama” amesema Mhandisi Sangweni.
Hata hivyo ameongeza kuwa mchakato wa kuhama kutoka katika matumizi ya Nishati inayochafua mazingira hadi nishati jadidifu unachukua zaidi ya miaka 30 ambapo amesema kuwa katika kipindi hicho cha mpito Nishati pekee inayoonekana ni nzuri, safi na inayofaa ni Gesi asilia.
“Gesi hii asilia tuliyoigundua tunaamini ndani ya miaka 30 itakuwa na soko kubwa kutokana kuwa kwa sasa ndio nishati pekee inayofaa na iliyokubalika “ ameongeza.
Kwa upande mwingine ameongeza kwa kuzungumzia namna ambavyo wananchi katika mradi huo watakavyopata fursa ya ajira na kushiriki katika utoaji wa uduma mbalimbali za kijamii.
“Sisi kama PURA tuna kitengo malum kinachojihusisha moja kwa moja kuhakikisha ushirikishwaji wa watanzania hususani wazawa unakuwa wa kiwango cha juu katika nyanja zote” amesisitiza Mhandisi Sangweni.