Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akitoa elimu ya ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma kwa wazazi wakati wa kampeni ya uchunguzi wa vimelea vya TB kwa watoto.
Mwenyekiti wa kijiji cha Angalia kata ya Mtina wilaya ya Tunduru Ali Mbanga akizungumza na baadhi ya akina mama wa kijiji hicho wakati wa kampeni ya uhamasishaji na uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto iliyofanywa na Hospitali ya wilaya Tunduru kitengo cha kifuka kikuu na ukoma.
Mratibu wa kifua Kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akiwa amemshika mtoto ambaye hakufahamika jina lake mara alipokuwa akitoa elimu ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa akina mama wa kijiji cha Angalia wilayani Tunduru.
Baadhi ya wanawake wa kijiji cha Angalia wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole(hayupo pichani)wakati wa zoezi la uchunguzi wa ugonjwa huo .
Na: Muhidin Amri,Tunduru
BAADHI ya Wakazi wa kijiji cha Angalia kata ya Mtina wilayani Tunduru,wameishukuru wizara ya afya kupitia Hospitali ya wilaya ya Tunduru chini ya kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa kuwafikishia huduma ya uchunguzi ya ugonjwa wa kifua kikuu katika kijiji chao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa TB kwa watoto wadogo na watu wazima walisema, hatua ya wizara kupeleka huduma hizo katika kijiji chao ni ukombozi mkubwa na itasaidia sana wananchi kutambua hali za afya zao.
Mwanahawa Abdala(45)alisema, katika kijiji hicho hakuna huduma yoyote ya afya,badala yake wananchi wanalazimika kwenda kijiji cha Mtina umbali wa km 7 kufuata huduma za matibabu ikiwamo ya uchunguzi wa afya zao.
Kwa mujibu wa Mwanahawa,kufikishwa kwa huduma za uchunguzi wa kifua kikuu na ukoma katika kijij chao na vijiji mbalimbali vya pembezoni inaonesha namna gani serikali inavyowajali na kuthamini wananchi wake kutokana na ukweli kwamba maeneo hayo hayafikiwi kwa urahisi na wataalam wa afya.
Alisema,katika kijiji hicho kuna watu wengi wanaougua ugonjwa huo na magonjwa mengine kwa muda mrefu, lakini wanashindwa kupata tiba sahihi kutokana na kutofikiwa na wataalam wa afya mara kwa mara.
Alisema, baadhi ya watu wamepoteza maisha kwa kutopata huduma ya uchunguzi wa afya zao na matibabu kwa wakati,hivyo kupelekwa kwa huduma ya uchunguzi wa TB itasaidia sana kuokoa maisha ya wananchi wengi hasa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
Habiba Said,ameiomba serikali kupeleka wataalam wa kutosha katika maeneo ya vijijini na kuboresha huduma za afya badala ya kupeleka nguvu kubwa mjini ambako ni rahisi kwa wananchi kupata na kufikiwa na huduma hizo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Angalia Ali Mbanga alisema,katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya,wameaanza ujenzi wa zahanati ambayo ipo hatua ya kupaua baada ya serikali kutoa fedha.
Hata hivyo,amewaomba wananchi na wadau mbalimbali kujitolea katika kazi ujenzi wa zahanati hiyo kwa kuwa serikali haiwezi kutekeleza kila jambo pekee yake kutokana na majukumu iliyonayo.
Ameupongeza uongozi wa Hospitali ya wilaya Tunduru kwa uamuzi wa kupeleka wataalam kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya za wananchi hususani wenye maradhi ya kifua kikuu na ukoma.
Kwa upande wake Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaa ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Tunduru ndiyo inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi wa kifua kikuu.
Alisema,hali hiyo inatokana na baadhi ya maeneo kuwa na makazi duni kutokana na ugumu wa maisha kwa wakazi wake na unywaji wa maziwa ya ng’ombe yasiyochemshwa vizuri.
Alisema,wanaendelea na kampeni ya kupambana na ugonjwa huo kwa watoto wadogo na watu wazima katika maeneo mbalimbali hasa vijijini na wale wanaobainika kukutwa na Tb wanaanzishiwa Dawa.
Dkt Kihongole ambaye ni mratibu wa tiba asili na mbadala wa wilaya hiyo,ameiomba jamii kutowatenga wagonjwa wa kifua kikuu,badala yake kuwapa ushirikiano na kuwapeleka katika vituo vya kutolea huduma ili waweze kupata matibabu yanayotolewa bure katika zahanati,vituo vya afya na Hospitali zote za serikali na binafsi hapa nchini.
Dkt Kihongole alitaja dalili za ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto ni kupungua uzito,kulia lia bila sababu,makuzi duni na kwa watu wazima kukohoa zaidi ya wiki mbili,kutokwa na jasho jingi nyakati za usiku,kukohoa damu,kukonda,kupungua uzito na kupoteza hamu ya kula.
Alisema,kinga mojawapo ya kuzuia kupata ugonjwa huo kwa watoto wadogo ni mama wajawazito kuhakikisha wanajifungulia Hospitali ambapo baada ya mtoto kuzaliwa anapata chanjo maalum ya kuzuia maambukizi ya magonjwa mbalimbali,kuepuka kukaa kwenye mikusanyiko,kuishi kwenye nyumba yenye mwanga na hewa ya kutosha.
Aliyataja makundi yaliyoko wenye hatari ya kupata ugonjwa huo ni wazee watoto wadogo,wafugaji,wasafiri,watu wanaoishi na virusi vya ukimwi,wafungwa na wanao kunywa pombe kupita kiasi.
MWISHO.