Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe atoa wito kwa watumishi wa Wakala wa Vipimo nchini kufanya kazi kwa bidii na uadilifu katika kumlinda mwananchi dhidi ya udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo leo Ijumaa tarehe 17 Septemba, 2021 alipotembelea ofisi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini na pia kupata fursa ya kutembelea ofisi za Wakala za Mikoa ya Temeke, Kinondoni, Ilala, Ofisi ya Vipimo ya bandarini iliyopo SIDO Vingunguti na baadaye kutembelea na kukagua kituo cha Upimaji cha Misugusugu kilichopo Mkoa wa Pwani.
Lengo la ziara hii ilikuwa na kukagua shughuli za utendaji wa Wakala wa Vipimo na kusikiliza changamoto zao ili kutafuta namna bora ya kuzitatua.
Katika taarifa yake Mhe. Kigahe ameanza kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kufanikisha maendeleo ya taifa letu, Aidha amesema kuwa wafanyabiashara wa Jumla na Rejareja wamekuwa wadanganyifu kwani wakinunua bidhaa viwandani wanapunguza ujazo wake halisi.
“Kumekuwa na tabia ya wanyabiashara kupunguza ujazo halisi wa bidhaa kwa lengo la kujipatia faida kubwa, nimejionea leo mifuko ya misumari iliyokamatwa na Wakala wa vipimo ambapo misumari hiyo ilikuwa imefungashwa katika kilo 50 lakini walipopima walikuta kilo 45, Aidha nimejionea bidhaa za ujenzi hasa nondo zisizo na ubora na pia nyigine zikiwa hazina jina la mtengenezaji, kwa sasa nchi yetu imeridhia mkataba wa eneo huru la Kibiashara (AfCTA) hivyo uaminifu na ubora wa bidhaa ni kitu cha msingi ili tuweze kulitumia vema soko hili ’’ Amesema Mhe. Kigahe.
Meneja wa Wakala wa Vipimo wa kituo cha Misugusugu ndugu Alban Kihula amesema kuwa kazi kubwa inayofanyika katika kituo hiki ni kazi ya uhakiki wa mita za maji, Uhakiki wa Tenki za Magari yabebayo vimiminika na uhakiki wa Mita za Umeme.
Ndugu Kihula ameongeza kuwa tangu kujengwa kwa kituo hiki ufanisi wa kiutendaji umeongezeka kwani awali walikuwa wakipima gari moja kwa siku nzima na sasa wanapima magari nne kwa mara moja na kwa siku wanauwezo wa kuhakiki magari Zaidi ya 70.
Mhe. Kigahe amemaliza kwa kusema kuwa watumishi wote wa Wakala wa Vipimo ndio wameshikilia maisha ya watanzania kwa kusimamia haki na usawa hivyo amewataka kuzingatia weledi na uadilifu katika utendaji wao wa kazi na atakayeenda kinyume atachukuliwa hatua kali za kisheria.