Na: Halfan Abdulkadir, Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi ameahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Maboresho ya mifumo ya taasisi za Haki jinai ambayo itatoa mwangaza juu kuboresha mifumo na taasisi zinazohusiana na masuala hayo kwa nia ya kupatikana haki nchini.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo September 09, 2023 Ikulu, Zanzibar alipokutana na tume hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Mohamed Othman Chande na Makamu Mwenyekiti Balozi Ombeni Sefue walipomkabidhi ripoti ya tume hiyo.
Rais Mwimyi Alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeyapokea mapendekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuleta mabadiliko na mageuzi makubwa kwa nia ya kupatikana kwa haki ufanisi.
Alisema utekelezaji wa mapendekezo hayo unaendana na kutegemeana na Taasisi zote za haki jinai za Tanzania Bara na Zanzibar.
Kadhalika Rais Mwinyi alizungumzia kuhusu ushirikiano mzuri uliopo baina ya taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa ya Zanzibar (ZAECA) na ya kupambana na dawa za kulevya, ambapo amsema Taasisi hizo zimepata msaada wa kujengewa uwezo na wenzao kutoka Bara kwa kupewa mafunzo.
“Bila shaka ni sahihi kabisa lazima kuwe na kubadilishana ujuzi na uzoefu, na ushirikiano wa karibu” alisifu Rais Dk. Mwinyi.
Kuhusu mahakama ya Rufani Bara kufanya kazi zake Zanzibar, alisema tayari suala hilo lipo mezani na linashughulikiwa.
Naye, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, alimueleza Dk. Mwinyi kwamba tume ilifanikiwa kuzifanyia kazi changamoto za taasisi 15 zilizopendekezwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwemo Jeshi la Polisi, Ofisi ya taifa ya Mashitaka, Jeshi la Magereza.
Taasisi nyengine ni Mamlaka ya kuzuia na kupambana na Rushwa, Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, Mahakama ya Tanzania, kitengo cha kudhibiti fedha haramu Uhamiaji, Ofisi ya Mkemea Mkuu wa Serikali na taasisi nyengine zinazohusu masuala ya jinai kwa kutathmni ushirikiano wa taasisi hizo na kuangalia nidhamu, mifumo ya ajira, viwango vya weledi, tume ya upandishaji vyeo, ufanisi mahusiano, nidhamu, ufanisi matumizi ya teknolojia na motisha.
Tume ya maboresho ya mifumo ya taasisi za Haki jinai imeundwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Januari 31 2023 na ilianza kazi zake mapema mwezi Februari kwa lengo la kutathmni mifumo ya haki jinai na kutathmini taasisi za haki jinai.