Meneja Masoko wa SGA Tanzania, Faustina Shoo na mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo Ziden Muta, wakimueleza jambo mmoja wa wanafunzi waliotembelea banda la kampuni hiyo wakati wa maonyesho ya nne ya teknolojia kwenye sekta ya madini yaliyofanyika mkoani Geita hivi karibuni.
KAMPUNI ya ulinzi ya SGA Security, ambayo ni kampuni inayoongoza kwa maswala ya ulinzi hapa nchini, imepongezwa kwa maendeleo yake ya kiteknolojia katika kutekeleza majukumu yake, ambayo yamepelekea kampuni hiyo kushinda tuzo kwenye maonyesho ya nne ya teknolojia kwenye sekta ya madini yaliyofanyika mkoani Geita hivi karibuni.
Katika maonyesho hayo ambayo yalifungliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kushirikisha makampuni zaidi ya 400 kutoka ndani na nje ya Tanzania, kampuni hiyo iliibuka mshindi katika kipengele cha teknolojia katika usafirishaji na usalama.
Akizungumzia mafanikio ya kampuni hiyo, Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko aliipongeza kampuni ya ulinzi ya SGA kwa maendeleo yake ya kiteknolojia ambayo alisema ni miaka mingi ambapo alisema ni mafanikio hayo ndiyo yaliyopelekea makampuni mengi ya madini kuwa na imani nayo na hivyo kuingia nayo mikataba ya ulinzi.
“Nitoe wito kwa uongozi wa kampuni hii kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na ushirikiano wa dhati na Serikali katika kuhakikishia ulinzi na usalama wa madini yetu dhidi wale wenye nia mbaya”, alisema.
Aidha Waziri Biteko aliishukuru kampuni ya ulinzi ya SGA kwa kukubali kuwa moja wapo ya wadhamini wa maonyesho hayo ya kila mwaka na mabyo hushirikisha wadau wa sekta ya madini kutoka ndani ya nje ya nchi ambao hufanya maonyesho yanayohusiana na shughuli wanazofanya katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita ambao ndiyo wenyeji wa maonyesho hayo, Rosemary Senyamule, aliipongeza kampuni ya ulinzi ya SGA kwa mafanikio hayo na kuwataka wachimbaji wadogo na wakubwa kutumia huduma za teknolojia ya hali ya juu katika nyanja za ulinzi zinazotolewa na kampuni hiyo.
“Kwa kushirikiana na kampuni ya SGA mtajihakikishia ufanisi zaidi na ulinzi wa kutosha wa mali zenu hata kama hamtakuwa ameneo ya ofisi zenu na machimboni”, alisema na kuongeza makampuni mengine hayana budi kuiga mfano wa SGA.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), Simon Shayo alipongeza kampuni ya ulinzi ya SGA kwa kuwekeza kwenye teknolojia ya ulinzi.
“Wengine wanadhani swala la ulinzi ni la mlinzi aliebeba rungu au silaha nyingine, la hasha kuna zaidi ya hayo; SGA imewekeza kwenye teknolojia ya kisasa katika ulinzi jambo linalowatofautisha na makampuni mengine”, alisema.
Akizungumza muda mfupi baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja Mauzo na Masoko wa kampuni ya ulinzi ya SGA, Faustina Shoo, alisema kuwa tuzo hiyo ni ishara ya ubora katika uwekezaji wa kiteknolojia ya ulinzi uliofanywa na kampuni hiyo.
“Tulifanya maonyesho ya jinsi teknolojia ya ulinzi inavyoweza kuwa suluhusisho katika kuimarisha ulinzi na usalama katika kuhdibiti mali za migodini sambamba na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi katika migodi na hivyo kufanya maeneo ya migodi kuwa sehemu salama pa kufanya kazi”, alisema na kuongeza uhakika wa namna hii huongeza tija na hivyo kuboresha Uchumi wa Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ulinzi ya SGA Tanzania, Eric Sambu, alielezea kufurahishwa kwake kutokana na mafanikio ya kampuni hiyo kutambuliwa na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, mafanikio ambayo alisema walistahili kuyapata kutokana na kujituma kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Aidha aliwapongeza wafanya kazi wa kampuni hiyo kwa kuonyesha uwezo na mafanikio ya kiteknolojia ya kampuni hiyo ya ulinzi ambayo alisema huwapa wateja wake thamani halisi ya huduma wanazolipia ili kuzipata.
Alisisitiza kuwa swala la usalama katika uwekezaji wa aina yoyote ni muhimu na kwamba kampuni ya SGA inajivunia kuchukua jukumu muhimu katika kuhakikisha ulinzi maeneo ya kazi kwa lengo la kukuza maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.
Alisema SGA ilikuwa kampuni ya kwanza kufanya kazi kama kampuni binafsi ya ulinzi nchini Tanzania na kwamba uongozi wa kampuni hiyo umethibitisha kuwa kujali maslahi ya wafanyikazi ni chanzo cha mafanikio ya kampuni yoyote haswa yale yanayojishughulihsa na maswala ya ulinzi.
SGA ndio kampuni kongwe binafsi ya ulinzi nchini iliyoanzishwa mwaka 1984 huku ikijulikana kama Group 4 Security. Kwa sasa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 5000 nchi nzima.
SGA ndio kampuni pekee ya ulinzi yenye cheti cha ISO 18788 – Security Operations Management System.
SGA Security inatoa huduma mbalimbali ikiwemo za ulinzi, alarm, huduma za fedha, ulinzi wa kielektroniki, huduma ya kusafirisha mizigona huduma nyinginezo.
Mwaka huu kampuni hiyo ilipokea tuzo baada ya kutangazwa mshindi wa jumla kama kampuni yenye rasilimali za kutosha na ya kuaminika (Most Equipped and Reliable Security Company of the Year, 2020) katika tuzo za chaguo la wateja (Consumer Choice Award).