Wanariadha wa mbio za mita 10000 kwa wavulana wakishindana leo Oktoba 9, 2021 jijini Arusha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, ametoa medali mbalimbali jijini Arusha leo Jumamosi, Oktoba 9, 2021, kwenye kilele cha Michezo ya Riadha Kitaifa, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina jambo na sekta ya michezo.
“Rais Samia ana jambo katika sekta ya michezo; Serikali yake inawekeza sana katika michezo kama sekta ya kimkakati kiuchumi, afya na utalii. Ndio maana ameongeza fedha za Timu za Taifa, ametoa asilimia 5 ya mapato ya michezo ya kubashiri matokeo kusaidia michezo na mwaka huu tunakwenda kurejesha Taifa Cup ambapo michezo itachezwa kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa na kuja kifaifa. Uwekezaji huu umeanza kuleta tija michezoni. Tuwe wamoja tu,” alisema Dkt. Abbasi.
Ametumia fursa hiyo pia kuzitakia kheri na kuzipongeza timu mbalimbali za Tanzania ambazo wiki hii na leo zinacheza/zimetwaa ubingwa wa aina mbalimbali; Twiga Stars na Tanzanite Ladies(U20) leo zinashuka dimbani Twiga ikiwania ubingwa katika fainali za COSAFA kule Afrika Kusini na Tanzanite ikicheza na Eritrea Dar kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia.
Ameitakia kheri Taifa Stars inayoshuka uwanjani kesho nchini Benin na ameipongeza Timu ya Taifa ya Kriketi U19 ambayo imeshika nafasi ya tatu Afrika katika mashindano ya Afrika yaliyomalizika juzi nchini Rwanda.
Katika mashindano hayo Failuna Matanga kutoka Arusha ambaye aliiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Olympik kwa mbio ndefu kwa upande wa wanawke ndiye ameibuka mshindi wa kwanza kwa mbio za mita 10000 na kufuatiwa na Natalia Elisante kutoka Unguja na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Maliseline Issa kutoka Arusha
Kwa apande wa wavulana kwa mbio hizo hizo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Faraja Damas kutoka Arusha, wakati nafasi ya pili ilichukuliwa na Inyasi Sulle kutoka Arusha na nafasi ya tatu kwenda kwa Aphonce Simbu kutoka Singida.
Kwa upande wa kurusha tufe Unguja ndiyo walioutawala mchezo huo ambapo washindi wote watatu walitoka huko. Washindi hao ni Tama Jaha Saburi aliyeshika nafasi ya kwanza, Lulu r. Kanua nafasi ya pili na Fatma Hamis aliyeshika nafasi ya tatu.
Kwa upande wa kurusha kisahani Joyce Mwang’amba kutoka Dodoma ndiye aliyeibuka mshindi wa kwanza akifuatiwa na Lulu Richard kutoka Unguja na Fatma Hamis aliyeshika nafasi ya tatu kutoka Unguja