MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewahimiza wananchi kuchangamkia Mpango wa kitaifa wa hifadhi ya Jamii kwa sekta isiyo rasmi unaotoa fursa kwa mtu mwenye shughuli halali inayomuingizia kipato kutenga sehemu ya kipato chake na kukiwekeza NSSF kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Hayo yamesemwa na Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Bw. Deus Jandwa, wakati akizungumza na waandsihi wa habari kwenye banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Tanzania 2023 yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini humo.
“Mfumo huu ni mwepesi, rahisi na wezeshi, unaotoa fursa kwa mwananchi kujiwekea akiba kidogo kidogo kulingana na kipato chake.” Alisema Bw. Jandwa
Alisema mpango huu ambao umewekwa na Serikali ili kumuwezesha mwananchi mwenye kipato kuendelea kujenga tabia ya kutenga sehemu ya kipato halali kujiwekea akiba ili panapotokea majanga au mtu anapofikia mahali ambapo hawezi kumudu kutekeleza majukumu yake ya kujiingizia kipato akiba hiyo ndiyo itakuwa mkombozi wake.
“Tunaamini makuzi yetu yanaanza utotoni kwa kulelewa na wazazi, ndugu au jamaa, lakini itafika wakati maisha yako yatasimamiwa na wewe mwenyewe na hasa kuanzia umri wa kustaafu wa miaka 55 na kuendelea, hapa suala la kujilea wewe mwenyewe linaanza kupungua na unahitaji kuelelewa na atakayekulea kwa uhakika ni akiba uliyojiwekea kupitia NSSF.” Alifafanua Bw. Jandwa.
Awali Afisa Uhusiano Mkuu wa NSSF, Bi. Janet Ezekiel alisema watatumia Maonesho hayo kuhakikisha kwamba kundi kubwa la wale ambao wamejiajiri wenyewe wanafikiwa kwa upana wake ili kuhakikisha wanajiandikisha kwenye Mfuko.
“Watu wanaotutembelea hapa tunawaelimisha na kuwaandikisha lakini pia timu yetu inapita maeneo mbalimbali kwenye viwanja hivi kwa nia ya kukutana na wajasiriamali na kuwaelimisha umuhimu wa kujiunga na Mfuko.” Alifafanua Bi. Ezekiel.
Alisema utaratibu wa mwanachama kuchangia ni rafiki unaomuwezesha mwanachama kumudu kuweka akiba.
“Viwango vya kuchangia ni himilivu, kima cha chini ni shilingi elfu 20,000/= na si lazima utoe fedha hizo kwa mkupuo, unaweza kutoa kidogokidogo kuanzia shilingi elfu 1,000/= na kuendelea bilashaka inapofika mwisho wa mwezi unakuwa umekamilisha malipo hayo.” Alibainisha
Alisema mfumo wa kuchangia pia ni rahisi mwanachama anapewa namba ya malipo na anaweza kulipia kupitia mitandao ya kifedha (mawakala wa mabenki na mitandao ya simu) au simu yake binafsi ya mkononi.
Akizungumzia huduma zitolewazo kwenye banda hilo, Bi. Ezekiel alisema mwanachama anapofika ataweza kupata taarifa za michango yake, taarifa za mafao, taarifa za uwekezaji, wastaafu kujihakiki lakini pia kuandikisha wanachama wakiwemo waajiri lakini pia wajasiriamali.
“Tunawakaribisha wakulima, wavuvi, wafugaji, mama lishe, bodaboda na wale wote wanaofanya shughhuli halali za kujiingizia kipato, kutembelea banda letu ili waweze kujua fursa zinazopatikana kwenye Mfuko.” Alifafanua.
Mmoja wa wanachama wa NSSF Bw. Brawn Msigwa aliyefika kwenye banda hilo, alisema akiwa kama kijana, anao wajibu wa kuanza kujiwekea akiba kwani pindi nguvu za kufanya kazi zitakapopungua akiba aliyojiwekea kidogo kidogo ndiyo itakayomsaidia pindi atakapostaafu.
“Asilimia kubwa ya fedha tunayopokea mwisho wa mwezi inakwenda kwenye mipango ya kila siku na inaisha yote hivyo ukiweza kujiwekea akiba NSSF ndiyo itakusaidia utakapostaafu.” Alisema.
Mwanachama huyo alipongeza huduma ya NSSF taarifa inayopatikana kupitia mtandao, kwani inafanya maisha kuwa rahisi.
“Nilikuwa na changamoto kidogo ya michango yangu ya kila mwisho wa mwezi, nimeelekezwa kupakua NSSF taarifa App, nimeweza kuona michango yangu moja kwa moja.” Alifafanua Bw. Msigwa
NSSF YAENDELEA KUTOA HUDUMA NANENANE KIMKOA MOROGORO
NSSF YAENDELEA KUTOA HUDUMA NANENANE KIMKOA ARUSHA.
Wananchi wakiandikishwa kuwa wanachama wa NSSF baada ya kupatiwa elimu ya hifadhi ya jamii walipotembelea banda la Mfuko katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo maarufu kama Nane nane yenye kauli mbiu “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula” yanayoendelea katika viwanja vya Nanenane Mjini Arusha.
NSSF YAENDELEA KUTOA HUDUMA NANENANE KIMKOA SIMIYU