Mratibu wa Mafunzo Chuo Cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT)) Tulla Mwigune, (kushoto), akizungumza na wanafunzi waliotembelea Banda la Benki hiyo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Mratibu wa Mafunzo Chuo Cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT)) Tulla Mwigune, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati wa mahojiano yaliyofanyika katika Banda la BoT, kwenye Maonesho ya Nanenane Jijini Mbeya.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Mwandishi wetu, MBEYA
Mratibu wa Mafunzo Chuo Cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT)) Tulla Mwigune, amesema kuwa Chuo hicho kimejiandaa kikamilifu katika kuhakikisha wanafunzi wote watakaopata nafasi ya kujiunga na Chuo hicho mwaka wa masomo 2023/2024 wanapokelewa bila changamoto yeyote.
Mwigune ameyasema hayo leo Agosti 4, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Amesema kuwa, baada ya kupokea maombi hayo watayachakata ili kuwapata wale wenye sifa ya kujiunga na Chuo na kupatiwa taarifa rasmi kwa ajili ya kuanza maandalizi.
“Baada ya kupokea maombi tutayachakata, wale ambao wamechaguliwa watatumiwa taarifa maalum kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kujiunga na Chuo” amesema Mwingine.
Ameeleza, wapo kwenye maonesho hayo ili kutoa elimu kwa wananchi na kwamba, kuna vijana wengi wamekuwa wakifika kupata maelezo juu ya kozi mbalimbali wanazozitoa, na kufahamu fursa nyingine zinazopatikana katika Chuo hicho.
“Wanafunzi wengi wamekuwa na changamoto ya kutojua kozi za kusoma, mfano kuna mwanafunzi anaweza kusema ili awe mhasibu lazima asome kozi za uhasibu, lakini haiko hivyo, ili uweze kuwa Afisa wa Benki kuna kozi ya Benki yenyewe ambayo ndani yake unasoma vitu halisia vinafanyofanyika Benki
“Tunavyoongelea Benki kuna vitengo mbalimbali, tukianza na huduma kwa mteja, kuna sehemu inayohusika na mikopo, pia kuna uhasibu ambao vijana wengi ndi wanaijua sasa lakini haya maeneo yote mtu anaweza akasoma kupitia hii kozi ya Benki, hivyo basi tunawakaribisha wanafunzi katika chuo chetu ili kupata elimu hiyo” ameeleza Tulla.
Aidha amesema kuwa Benki kuu imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu mbalimbali chuoni hapo, ambapo wanafunzi wote watakaopata nafasi ya kusoma katika Chuo hicho wataweza kusoma kwa utulivu na kwamba, Chuo kimejitosheleza kwa madarasa ya kutosha pamoja na Maktaba ya kisasa yenye vitabu vipya, na maeneo tulivu ya kujisomea.