(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM
Wito umetolewa kwa wananchi wa kada mbalimbali wakiwemo wadau wa elimu chini, kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe, katika kukabilina na uhaba wa mabweni ya wasichana katika Kampasi ya Mbeya, kwa kuchangia fedha ili kuongeza kasi ya ujenzi wa mabweni hayo yanayotarajia kujengwa na Chuo hicho Jijini Mbeya.
Wito huo umetolewa Julai 2,2023 na Makamu Mkuu Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) Prof. Lughano Kusiluka alipotembelea Banda la Chuo Kikuu Mzumbe kwenye Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Kibiashara (Sabasaba) yanayofanyika Jijini Dar es Salaam.
Prof. Kusiluka amesema kuwa serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mtoto wa kike analindwa, ikiwa ni pamoja na kuwajengea mabweni ya kuishi na kwamba, hiyo imekuwa moja ya ajenda za Taifa ya kuhakikisha wanawake wanapata fursa ya kusoma katika mazingira rafiki.
“tutaendelea kutafuta fedha sehemu nyengine kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi ili kuhakikisha wanasoma katika mazingira rafiki” amesema Prof. Kusiluka.
Amekipongeza Chuo hicho kwa kuanzisha harambee ya kukusanya fedha zitakazosaidia kujengwa kwa Mabweni ya wasichana katika Kampasi ya Mbeya, ambapo ameahidi kuchangia Shilingi Milioni moja katika ujenzi huo.
Katiaka hatua nyingine, Prof. Kusiluka hakusita kutoa pongezi zake kwa Chuo hicho kwa namna walivyojipanga kikamilifu kushiriki katika maonesho ya Sabasaba mwaka huu, na kuongeza kuwa, hata Banda lao limekuwa na muonekano mzuri.
“Nimetembelea Mabanda mengi katika maonesho ya sabasaba lakini Chuo Kikuu Mzumbe wamekuwa na Banda bora” amesema Prof. Kusiluka.