Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kuwa katika jitihada za kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa sera ya fedha, inatarajia kubadilisha mfumo wa sasa wa utekelezaji wa sera ya fedha, ambao unatumia ujazi wa fedha, na kuanza kutumia mfumo mpya unaotumia riba ya Benki Kuu (Central Bank Policy Rate) katika kusimamia malengo mapana ya kiuchumi ya kudumisha utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi kuanzia mwezi Januari 2024. Mfumo huu ulianza kutumika duniani mwaka 1990 ambapo hadi sasa unatumiwa na Benki Kuu za nchi 45.
Utekelezaji wa Mfumo wa Riba ya Benki Kuu umeonesha matokeo mazuri katika usimamizi wa sera ya fedha na kuimarisha misingi ya utekelezaji wake katika mazingira ya uwazi katika nchi zinazotumia mfumo huu. Maelezo na ufafanuzi zaidi kuhusu mfumo huu mpya wa sera ya fedha yameambatishwa na taarifa hii kama Kiambatisho Na. I. Aidha, maelezo ya ziada yanapatikana pia katika Tamko la Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania ya 2023/24 na Tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania: www.bot.go.tz/Publications/Filter/48?lang=sw
Kwa muktadha huu, ili kuhakikisha kuwa mabadiliko haya yanafanyika kwa ufanisi, Benki Kuu ya Tanzania imeandaa Mwongozo wa utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia riba ya Benki Kuu ambao umeambatishwa na taarifa hii kama Kiambatisho Na. II. Madhumuni ya Mwongozo huu ni kutoa taarifa muhimu kwa wadau ili kuongeza uelewa kuhusu sera ya fedha, hatua na taratibu zinazohusika katika mfumo mpya wa sera ya fedha kwa kutumia riba. Mwongozo huu utasaidia kutoa ufafanuzi kuhusu uandaaji na utekelezaji wa sera ya fedha ili kuwezesha wadau kupangilia shughuli zao na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera ya fedha.
Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kushirikisha wadau mbalimbali kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya mfumo mpya wa sera ya fedha na hivyo kuwezesha kufikia malengo ya sera ya fedha ya kudumisha utulivu wa bei na kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi.
GAVANA
BENKI KUU YA TANZANIA