KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema Chama hicho kitahakikisha kinaendelea kuweka msukumo na kusimamia katika kuwalinda wazalishaji wa ndani kwa nguvu zetu zote huku akitoa rai ya mbolea inayozalisha nchini ipewe nafasi kubwa katika soko la ndani.
Chongolo ameyasema hayo leo alipotembelea kiwanda cha mbolea asili cha ITRACOM FERTILIZERS LTD kilichopo Nala wakati wa ziara ya kikazi ya siku nane ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu sambamba na kusikiliza kero za wananchi inayomalizika leo mkoani hapa.
Amesema anapongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa hatua mbalimbali ambazo wanaendelea kuchukua katika uzalishaji wa mbolea asili kwani wamepiga hatua kubwa ukilinganisha na hapo nyuma, hivyo kazi iliyobaki ni kuendelea kuwatimia moyo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya.
Wakati anaanza kuzungumza Chongolo amesema akiwa kwenye kiwanda hicho amepata muda mwingi kusikiliza maelezo mbalimbali na lengo la kufanya hivyo ni kujifunza maana wao ndio wasimamizi wa Ilani.
“Wenzetu wamekuwa wakiumiza kichwa kufanya mambo yatokee, hivyo n sisi tunatakiwa kuumiza kichwa ili mambo yatekelezeke.Niwapongeze kwa kazi kubwa wanayoifanya ,sasa hivi kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha wanapata soko la ndani kwa kiwango kikubwa lakini tuwatengeneze miundombinu ya kupata soko la nje ili wawe chanzo cha kuingiza fedha za kigeni, na ili tutengeneze hivyo lazima uwe na mkakati ambao utafanikisha hayo.
“Kama mbolea hii inafanya vizuri na inaendelea kufanyiwa utafiti inafanya vizuri msuko wa kwanza uwe wa tujiwekee kinga kwamba kwasababu tayari tuna uzalishaji ndani mbole ya kiwango hiki mpaka asilimia hii itoke ndani halafu asilimia kidogo iliyobakia itoke nje kwa wale watu wenye kasumbuka ya kupenda vya kigeni hata kama vya kwetu ni bora,”amesema Chongolo.
Hata hivyo amesema kasumba hiyo inaisha taratibu kutokana na kuona uwenzao wanavyofanya vizuri zaidi. “Kwa hiyo cha kwanza nirejee maneno yangu niliyosema mwaka jana tunapoweka mpango wa ruzuku tuweke msuko wa matumizi ya mbolea ya ndani ili kutengeneza msukumo wa ajira zetu kulindwa , wawekezaji wa ndani kulindwa lakini na tija ya kiuchumi kulindwa.
“Pia twende kwenye hatua ya pili kufikiria kuagiza kama usambazaji utaonekana kuwa changamoto , tuhamasishe wawekezaji wa ndani lakini sisi tuwe chanzo cha kutangaza hii mbolea hata kama si ya Serikali kwani ikienda kuuzwa nje na mahitaji yakawa makubwa wanaonufaika ni vijana wetu wenye ajira hapa.
“Leo hii najua Wagogo wote wenye ng’ombe hakuna mbolea kwenye zizi , zote zinakuja hapa , kesho wataenda Manyara ,Singida, Tabora na kesho kutwa wataenda Arusha na maeneo mengine, maana yake ni nini ?Maana yake mtu aliyekuwa anajua anachunga ng’ombe na kufuga ng’ombe kwa ajili ya nyama sasa atajua umuhimu wa mbolea kwasababu tayari soko lipo .
“Hiyo ni tija kubwa ambayo wengine bado hawajaiangalia ni kwa namna gani inaendelea kutanua wigo wa ajira, kwasababu ajira ni kitu chochote unachokuingiza kipato, kama una mbolea ya samadi kuna mtu anahiitaji ukiuza ndio ajira yenyewe , kwa hiyo ni vitu vinavyoleta matokeo kwenye uchumi.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mbolea Itracom Ndugu Nduwimana Nazaire amesema hivi sasa kiwanda kina jumla wafanyakazi wa wapatao 1000, kati ya hao 380 wana ajira za kudumu na wako moja kwa moja kwenye uzalishaji kiwandani idadi ilibaki wako katika idara ya ujenzi.
“Kwa wenye ajira za kudumu kuna Watanzania 208 na Warundi 172. Baada ya kumaliza usimikaji wa mitambo yote kiwanda zitatolewa ajira kwa Watanzania takribani 2048 wa kada mbali mbali kufanya kazi kiwandani ili kufikia lengo la uzalishaji wa Tani 1,000,000 za mbolea kwa mwaka”,amesema Nazaire
Amesema Kiwanda cha kuchanganya mbolea kitaajiri takriban Watanzania 75. Mtambo kuzalisha chokaa utaajiri takriban Warundi 10 na Watanzania 54 wakati Kiwanda cha kuchakata fosfeti mkoani Manyara, Vilima Vitatu kinachoendelea kujengwa kitaajiri takribani Warundi 20 na Watanzania 123 wanaofanya kazi katika kiwanda hicho ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023.
“Hivyo, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2023, ITRACOM FERTILIZERS LTD itakuwa imeajiri takribani wafanyakazi 3067 (Warundi 288 na Watanzania 2779)”,amesema Nazaire.
CREDIT: Michuzi Blg
Katibu Mkuu wa CCM Komredi Daniel Chongolo akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mbolea Itracom Ndugu Nduwimana Nazaire