Dakar, Senegal
Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania June 13, 2023 amehutubia kwa njia ya mtandao Mkutano wa Kimataifa wa Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia (EITI) unaondelea Jijini Dakar nchini Senegal chini ya udhamini wa Rais Macky Sall, Bodi ya EITI na wadau wa sekta za uziduaji.
Katika hotuba yake fupi aliyowasilisha mbele ya washiriki zaidi ya 1,500 toka nchi zaidi ya 90; Rais Samia alisistiza umuhimu wa wavunaji wa Raslimali za madini kuhakikisha kuwa Uwekezaji wao unawanufaisha wananchi wanaoishi katika maeneo husika na taifa kupitia uwekaji wazi wa kumbukumbu za uzalishaji wao einazoonyesha mchango stahiki wanaochangia jamii na pato la taifa. Kwa sasa nchi 57 duniani ni wanachama hai wa EITI na nchi yetu Tanzania tukiwa miongoni mwao kupitia taasisi yetu ya TEITI.
Ujumbe wa Tanzania uliowakilisha taifa letu kwenye Mkutano huo uliongozwa na Dkt. Steven KIRUSWA, Naibu Waziri wa Madini na wajumbe sita ambao ni Dkt. Abdulrahaman Mwanga, Kamishna wa Madini, Mhe. Danstan Kitandula, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, pamoja na Mhe. Jesica Kishoa, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Wengine ni Bi Mariam Mgaya, Kaimu Mtendaji wa TEITI, Ndugu Ludovic Utouh, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI na Ndugu Adam Anthony, Mjumbe wa Kamati ya TEITI.
Mkutano huu ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu Mkuu wa Senegal kwa niaba ya Rais Macky Sall pia ulihudhuriwa na Mawaziri wakuu toka nchi mbali mbali sambamba na waliohudhuria kwa njia ya mtandao akiweko Mh. Tony Blair, Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza.
Mkutano huu utaendelea kesho tarehe 14/6/2023 ambapo ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Dkt. KIRUSWA utawasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya Madini Mkakati.