Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza na Mbunge wa Tabora Kaskazini, Mhe. Athumani Almas Maige, mara baada ya semina iliyofanyika leo jijini Dodoma katika Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa.
Benki Kuu ya Tanzania imetoa semina kwa waheshimiwa Wabunge jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa uchumi wa dunia, athari za mwenendo huo kwenye upatikanaji wa fedha za kigeni, na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu kukabiliana na hali ya fedha za kigeni nchini.
Katika wasilisho hizo imeelezwa kwamba kuanzia mwaka 2022 hadi hivi sasa, mwenendo wa uchumi wa dunia umekuwa sio wa kuridhisha kutokana na kukabiliwa athari za UVIKO-19, vita ya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabianchi.
Changamoto hizo zimeathiri mwenendo wa uchumi nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania na kwamba serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.
Dkt. Missango alisema athari za mwenendo wa uchumi wa dunia kwa fedha za kigeni nchini ni pamoja na kuongezeka kwa nakisi ya urari wa malipo kwa asilimia 127.3 katika kipindi cha mwaka mmoja hadi Disemba 2022 kutoka mwaka 2021 na nakisi ya urari wa malipo ni hasi kwa kiasi cha dola bilioni 5.4 kutoka dola bilioni 2.4 mwaka 2022.
Kutokana na hali hiyo, alisema tangu mwaka 2022, fedha za kigeni nchini zimekuwa zikipungua kutokana na kupungua kwa fedha za kigeni kutoka vyanzo mbalimbali kutokana na sera zilizochukuliwa na benki kuu za nchi zilizoendelea, uwekezaji katika masoko ya fedha kuelekea nchini Marekani na hivyo kusababisha kupungua kwa mikopo na misaada kutoka nchi za nje.
Aidha, ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mwaka 2022, kama za mafuta, chakula na mbolea, kugharamia miradi ya maendeleo na kulipa madeni ya nje, kumechangia pia kupungua kwa fedha za kigeniHatua zinazochukuliwa na Benki Kuu kukabili hali hiyo ni pamoja na kuendelea kuuza dola milioni 2 kila siku katika soko, kununua dhahabu yenye thamani ya dola milioni 280 kwa mwaka, sawa na tani 6 ili kukuza akiba ya fedha za kigeni. Mpaka sasa imeshanunua kilo 418 kutoka kwa Serikali.
Hatua zingine ni kupata fedha za kigeni kutoka kwa mabenki ya ndani na nje kwa njia ya currency swap, kuuza akiba ya Kwacha za Zambia zilizopo kwenye akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania iliyopo Benki Kuu ya Zambia, kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kupunguza ukwasi wa shilingi kwenye uchumi, kutoa leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo mengi nchini ili kuongeza fedha za kigeni kwenye mzunguko rasmi.
Aidha, hivi karibuni Benki Kuu imetoa sekula kwa mabenki ambayo imeanza kutumika tarehe 1 Juni 2023 yenye lengo la kudhibiti fedha za kigeni.Matarajio ni kuanza kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutokana na kwamba bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta, zinaendelea kushuka hivyo mahitaji ya fedha za kigeni yatapungua.
Aidha, kipindi cha Julai hadi Septemba ni msimu wa utalii na mauzo ya mazao ya biashara, hivyo inatarajiwa kwamba upatikanaji wa fedha za kigeni utaongezeka.
Pamoja na hatua na hali hiyo, wananchi wamehimizwa kuongeza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kutumia fedha za kigeni zilizopo kwa uangalifu kwa kuagiza bidhaa ambazo ni muhimu na zisizozalishwa hapa nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliana na changamoto hii ya dunia.
Wengine waliokuwa katika ujumbe wa Benki Kuu walikuwa ni Meneja Idara ya Masoko ya Ndani, Bw. Lameck Kakulu na Meneja Idara ya Mawasiliano, Bi. Victoria Msina.
Pamoja na Benki Kuu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), pia walifanya mawasilisho kwa Waheshimiwa wabunge kuhusu shughuli zao, na baadae Wabunge walipata nafasi ya kuchangia na kuuliza maswali