Na: Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewajulia hali majeruhi 10 wanaoendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya Temeke waliojeruhiwa kutokana na tukio la kukanyagana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wakijiandaa kuingia kutazama mechi kati ya Yanga na USM Alger ya nchini Algeria katika mchezo wa Kwanza wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, uliocheza Mei 28, 2023.
Mhe. Chana alipokea taarifa kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Joseph Gasper Kimaro kwamba, walipokea majeruhi 30 ambapo wanaume walikua 18, Wanawake 10 na mtoto Mmoja ambapo mgonjwa mmoja alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu.
Ameeleza kuwa mpaka sasa wamebakiwa na wagonjwa 10 na wote wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika.
Mhe. Chana katika ziara hiyo aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, Naibu Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, Katibu Mkuu, Bw. Saidi Yakubu, Mkuu wa Wilaya Mhe. Mwanahamisi Munkunda.
Credit: Mzalendo Blog