WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapongeza Wakuu wote wa Mikoa na Wakuu wote wa Wilaya nchini kwa kazi nzuri waliyofanya ya kusimamia miradi ya maendeleo na hasa ujenzi wa madarasa.
“Kupitia kwako Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya waliopo hapa, nitoe pongezi kwa Wakuu wengine wa Mikoa na Wilaya kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya maendeleo. Hii ni pamoja na usimamizi wa fedha, uratibu wa matumizi ya fedha hizo na usimamizi wa kuhakikisha miradi inakuwa ya viwango,” amesema.
Ametoa pongezi hizo leo mchana (Jumapili, Januari 02, 2022) wakati akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali wa mkoa wa Ruvuma kwenye uwanja wa ndege wa Ruhuwiko, wilayani Songea mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo.
Waziri Mkuu amesema amefanya ziara kwenye mikoa ya Mbeya, Lindi, Dodoma, Dar es Salaam na sasa yuko Ruvuma na amejionea kazi nzuri iliyofanyika. Amesema ifikapo Januari 5, usafi ufanyike kwenye madarasa yaliyojengwa ili yakabidhiwe kwa Wakuu wa Shule.
“Ari ya usimamizi wa ujenzi iliyooneshwa katika miradi hii, ikifanyika kwenye miradi mingine yote, ni lazima nchi hii itafika mbali. Tunatambua katika miradi mikubwa kama hii hapakosi changamoto, lakini kuna wengine ambao wamefanya kazi nzuri hadi kubakiza fedha.”
Amewataka wasimamie miradi iliyosalia ya afya, maji na ujenzi wa barabara (TARURA) kwa mtindo huohuo. Ametumia fursa hiyo kumwahidi Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Bw. Oddo Mwisho kwa niaba ya wenzake, kwamba Serikali itasimamia vizuri miradi mingine kama ilivyosimamia miradi hii ya maendeleo.