Mbunge wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi ambaye pia ni Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Jakaya Kikwete,Mama Salma Kikwete (kulia) , Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Coca-Cola Unguu Sulai( watatu kulia) Meneja Masoko wa Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba( wa tatu kushoto)Meneja Uhusiano wa Coca-Cola Salum Nasoro(wa pili kushoto) wakiwa na mmoja ya Wanawake mwenye ulemavu(wa kwanza kushoto) wakimkabidhi jiko la Oryx pamoja na mtungi wake wenye kilo 15 akiwakilisha wanawake wanaojihusisha na Mama lishe jijini Dar es Salaam . Mitungi 100 ya Oryx na majiko yake imetolewa bure kwa Mama lishe hao kupitia programu ya Mwanamke Shujaa inayoratibiwa na kuandaliwa na Kampuni ya Coca-Cola.
Meneja Masoko wa Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba akizungumza wakati wa tukio la kukabidhi mitungi 100 ya Oryx pamoja na majiko yake kwa Mama Lishe kupitia programu ya Mwanamke Shujaa inayoratibiwa na kuandaliwa na Kampuni ya Coca-Cola kwa lengo la kuwawezesha Wanawake kiuchumi.
Mama Salma Kikwete ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi akizungumza kabla ya kukabidhi mitungi ya gesi 100 pamoja na majiko yake kwa wanawake wanaojihusisha na shughuli za Mama Lishe ambao wamepata majiko hayo kupitia programu ya Mwanamke Shujaa inayoratibiwa na Kampuni ya Coca-Cola Kwanza.
Na: Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi ambaye pia ni Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Dk.Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete ameipongeza Kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa kugawa bure mitungi ya gesi 100 yenye ujazo wa kilo 15 pamoja na majiko yake kwa Mama Lishe jijini Dar es Salaam.
Oryx Gas Tanzania wametoa majiko hayo bure kupitia programu maalum ya Mwanamke Shujaa inayoratibiwa na Kampuni ya Coca-Cola Kwanza ambayo kwa muda mrefu imekuwa na programu hiyo yenye lengo la kumuwezesha mwanamke wa Tanzania sambamba na kumjengea kujiamini na kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa tukio la kukabidhi majiko ya Oryx Gas na majiko, meza pamoja na kofia za Mama lishe,Mama Salma Kikwete amesema kitendo hicho ni muhimu katika ustawi wa wanawake na kinapaswa kufungwa mkono na wadau wote wa maendeleo nchini.
“Leo hii kupitia programu hii ya Mwanamke Shujaa zaidi ya wanawake 350 wanaojishughulisha na shughuli za chakula Kwa maana ya Mama Lishe wamepata mafunzo ya ujasiriamali,utunzaji wa kumbukumbu pamoja na mafunzo ya saikolojia.Baada ya mafunzo haya wanapatiwa vifaa ambavyo vitaongeza tija kwenye shughuli zao.
“Hili ni jambo jema la kuigwa na wadau wengine wa maendeleo,naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Coca-cola Kwanza kwa kuwa na programu ya Mwanamke Shujaa, nawapongeza sana Oryx Gasi Tanzania kwa kutoa majiko ya gesi na mitungi yake Kwa akina Mama hawa ambao kweli ni Wanawake Shujaa.
Awali Meneja Masoko wa Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Araman Benoite,amesema Tanzania inakabiliwa na uharibifu wa misitu na ila tusipokuwa makini nchini itageuka kuwa jangwa kwani takwimu zilizopo Sasa hivi zinaonesha ni asilimia 5 tu ya wananchi wanatumia nishati ya gesi na wengine kama asilimia 90 wanatumia kuni na mkaa.
“Sisi kama Oryx Gas katika kujibu changamoto hiyo tumeaungana na Mwanamke Shujaa ambayo ni programu ya Coca-cola ambayo ni nzuri sana kwetu,tumeona lazima tuunge mkono jitihada zote za Kampuni hiyo kusaidia wajasiriamali Wanawake,kumbuka kwamba wajasiriamali ambao wanafanya shughuli za upishi ni kundi kubwa ambalo muda mwingi linatumia kuni na mkaa
“Kuni na mkaa madhara yake ni makubwa,sio tu kiuchumi bali kiafya pia wanasema karibu asilimia 30 ya Watanzania wanaugua magonjwa ya hewa,pumzi na mapafu ,sio sigara tu hata kuni na mkaa ambao tunavuta kila siku,sasa pata picha wewe uko kwenye jiko la mkaa muda wote itakuaje ndani ya miaka 10 ijayo.
“Hivyo Oryx Gas tumekuwa na programu mbalimbali na ndani ya miaka miwili tumesaidia makundi mbalimbali ya Wanawake karibia 5000 kwa kuwapatia nishati safi ya gesi ya kupikia kwa maana ya mitungi ya gesi na majiko yake,”amesema Ndomba.
Amesema waaendeleza kadiri inavyowezekana kufika watu wengi nchi nzima na wanafanya hivyo ili kuonesha mfano kwamba njia nzuri ya maisha ni kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na kuni na mkaa ,hivyo Kwa kuwapatia mitungi na majiko Mama lishe hao wanaamini watakuwa mfano wa kuigwa na wengine na hivyo kuachana na kuni na mkaa.
“Oryx tumekuwa na jitihada nyingi sana za kimafunzo na kuendeleza watu,tuna programu yetu inayosema elimu na uwezeshaji katika jamii kutunza mazingira, tunatoa mafunzo kwa watu mbalimbali.Pia Oryx Gas inaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhifadhi mazingira.
“Tukumbuke mwaka jana kwenye mkutano wa matumizi ya nishati safi ya kupikia alitamani sana kufika mwaka 2030 asilimia ya Watanzania wanaohama kutoka kuni ifike angalau 80 ,itoke tano mpaka 80, kwa hiyo sisi tumeibeba hii ajenda kwa mikono yote miwili na tunaisukuma mbele kwa kuhakikisha kila mtanzania anapata kutumia nishati ya gesi.”
Mwisho