Na: Steven Nyamiti, WM.
NAIBU Waziri wa Madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido Mkoa wa Arusha Dkt.Steven Kiruswa, ametoa agizo kwa mmiliki wa Mgodi wa Paramaount Ltd unaofanya shughuli za uchimbaji katika Kijiji Cha Sinoniki na Kimwati katika tarafa ya Engarenaibor wilayani Longido kuhakikisha anafuata taratibu za upataji wa eneo la ardhi na kupitishwa kwenye mkutano Mkuu wa Kijiji.
Ameyasema hayo leo Januari 27, 2022 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Longido alipotembelea migodi iliyopo katika Kijiji cha Sinoniki na Kimwati Tarafa ya Engarenaibor yanapochimbwa madini ya vito aina ya Quartz na Spessatite na Kampuni ya Uchimbaji ya Paramount Ltd.
“Nimeona hapa Kimwati mmefuata utaratibu wote unaotakiwa,lakini Sinoniki hamjafuata taratibu naomba mkaliweke sawa kabla wizara haijachukua hatua kali za kisheria, lakini pia mkifuata taratibu mtaepuka migogoro na jamii,”amesema Dkt.Kiruswa.
Dkt.Kiruswa amewataka kufuata taratibu zote za kisheria ili kuepuka migogoro na jamii ikiwemo masuala ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kuweka makubaliano yenye kuonekana kwa jamii ikiwemo kusaidia miradi ya maendeleo.
“Nakuagiza Mwenyekiti wa Kijiji kaitisheni kikao cha Serikali ya Kijiji hata cha dharura na ifikapo wiki ijayo taarifa ya makubaliano hayo yawe yamefika kwa Mkuu wa Wilaya Longido na sisi wizarani tutapata na kuangalia kama yapo sawa,” amesema Dkt.Kiruswa.
Hata hivyo, amewashauri wawekezaji hao kufanya tafiti zaidi kabla ya kuanza uchimbaji au kuendelea kufanya uchimbaji kwa kukisia pasipo kuwa na uhakika pamoja na kuweka utaratibu wa kusoma taarifa za miradi waliyoitekeleza kwa jamii katika mikutano mikuu ya vijiji.
Katika hatua nyingine, amewataka kutumia utaalamu wa kuchimba madini ya vito ili kuepuka uharibifu wa mazingira na kueleza kuwa maeneo hayo ni maeneo ambayo hutumika kama korido ya wanyamapori na mifugo ya wananchi.
Dkt.Kiruswa amewapongeza wawekezaji hao kwa kutoa fursa kwa vijana wazawa katika migodi hiyo na kuwasisitiza kutoa fursa kwa wanawake kuchakata mawe ili waweze kujiinua kiuchumi pamoja na kusisitiza ulinzi wa madini hayo pasipo kutorosha kupeleka nchini jirani, kwani migodi hiyo ipo mpakani maeneo ya mipakani.
Naye, Ofisa Madini Mkoa wa Arusha, Mhandisi Alphonce Rikulamchu amesema wilaya hiyo ina jumla ya migodi 10 yenye leseni za uchimbaji mdogo (PML) na kati ya migodi hiyo mitano ipo katika Kata ya Mundarara yalipo madini aina ya Rubi na Kijiji cha Sinoniki mmoja yanapatikana madini aina ya Spessartite.
“Migodi mingine ipo katika Kijiji cha Matale unaochimba madini aina ya Sunstone na Quartz pamoja na migodi mitatu iliyopo Kijiji cha Kimwati inayochimba madini aina ya Rubi na Quartz,”amesema Alphonce.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sinoniki, Mbatiany Laizer amesema, mkutano Mkuu wa Kijiji kwa ajili ya kuazimia shughuli za uchimbaji kuanza kwa Kampuni ya Paramount Ltd umetokana na hali ya ukame uliopo na kupelekea wafugaji kuhama hama kutafuta malisho.
“Kila tukihitisha mkutano akidi haitimii, lakini tunatarajia hivi karibuni kupitisha tena,”amesema Laizer.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya uchimbaji ya Paramount Ltd, Zainali Bhimwali amesema, katika kutengeneza uhusiano mzuri na jamii hiyo, kampuni imefanikiwa kufungua barabara kwa ajili ya kuunganisha Kijiji cha Kimwati na Sinoniki na wanatarajia kukabidhi madawati 100 kwa ajili ya shule za msingi kwenye vijiji hivyo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema, ni lazima wawekezaji waheshimu Sheria, Kanuni na Taratibu ili wafanye shughuli za uchimbaji madini kwa tija. Amesema ni lazima pia waboreshe huduma za kijamii ili wananchi wa maeneo hayo waweze kunufaika na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
“Hairuhusiwi kuanza shughuli za uchimbaji bila kupita kwenye mkutano Mkuu wa Kijiji na kuridhia,” amesisitiza Dkt.Mwanga.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Nurdin Babu amesema, Serikali inahitaji wawekezaji lakini pia wanatakiwa kufuata taratibu za kisheria katika uwekezaji