Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo | Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi ya Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amefungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini yanayoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi w Elimu (ADEM) Bagamoyo Pwani.
Nombo amesisitiza wajumbe hao wa Bodi kuhakikisha wanasimamia uendeshaji wa vyuo vya ualimu ili vilete tija ya kuandaa walimu mahiri wataochagiza utoaji wa elimu bora nchini.
Akizungumza katika ufunguzi huo Prof. Carolyne Nombo amesema kipaumbele cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kusimamia masuala ya elimu umejikita katika kuzingatia ubora hivyo Bodi za Ushauri za Vyuo vya Ualimu nchini zinapaswa kusimamia upatikanaji wa walimu mahiri ambao watakwenda kutoa ujuzi mahiri kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali.
“Hii iwe ndio Dhamira yetu sote sisi tunaosimamia Sekta ya elimu nchini, Vyuo vya Ualimu vijikite katika kuandaa Walimu mahiri na wanaotosheleza katika ngazi zote, hivyo wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini wana dhima kubwa katika kuhakikisha dhamira hii inafikiwa“. Amesema Prof. Carolyne Nombo
Naye Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah akizungumza na Washiriki wa Mafunzo hayo katika ufunguzi huo amesema Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu -ADEM baada ya kupitia na kufanya uchambuzi wa namna Bodi za Vyuo vya Ualimu zinavyoendeshwa na kubaini mapungufu kadhaa, unaendesha mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo Wajumbe hao wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini katika masuala ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Vyuo vya Ualimu, kuyafahamu majukumu ya Bodi ya Ushauri, Uandaaji wa mpango mkakati wa chuo, na masuala ya Ufuatiliaji na namna ya kufanya tathimini ya utendaji kazi wa Vyuo vya Ualimu.
“Tumejipanga ili kuwajengea uwezo na kuwaongezea weledi katika Usimamizi wa vyuo vya Ualimu, hii itasaidia washiriki wa mafunzo haya waweze kuleta ubora katika vyuo vyetu na ubora kwa walimu wetu” Dkt. Siston Masanja, Mtendaji Mkuu wa ADEM.
Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi Fanisi wa Vyuo vya Ualimu yanafanyika kwa siku saba (7) ADEM Bagamoyo yakiwa na lengo la kuimarisha Usimamizi wa Vyuo vya Ualimu nchini ambapo wajumbe 308 wa Bodi za Vyuo vya Ualimu wanashiriki mafunzo hayo kutoka katika Vyuo 35 vya Ualimu.