Home BUSINESS WAISHUKURU PURA KWA KUPIGANIA USHIRIKI WA WATANZANIA

WAISHUKURU PURA KWA KUPIGANIA USHIRIKI WA WATANZANIA

Sehemu ya Wafanyakazi wa Kitanzania Walioajiriwa Katika Mradi wa Ukarabati wa Visima Songo Songo Mkoani Lindi.

Kazi Ya Ukarabati wa Visima Ikiendelea Songo Songo – Lindi

Watanzania wanaofanya kazi katika mradi wa ukarabati wa visima vya kuzalisha gesi asilia vilivyopo Songo Songo Mkoani Lindi wameishukuru Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa kupigania ushiriki wa watanzania watanzania katika miradi huo.

Shukrani hizo zimetolewa na wafanyakazi hao leo tarehe 17 Februari, 2022 wakati PURA ilipofanya ziara ya ukaguzi wa masuala ya ushiriki wa watanzania katika mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Bw. Wandiba Joseph Kibebe ambaye pia anafanya kazi kama Mchimbaji Msaidizi (Assistant Driller) katika mradi huo ameeleza kuwa PURA imefanya juhudi kubwa kuhakikisha kampuni ya Exalo Drilling SA kutoka Poland inayotekeleza mradi huo inatoa fursa kwa watanzania kushiriki kupitia ajira.

“Ni dhahiri kuwa kama si PURA kusimama kidete kuhakikisha watanzania wanapewa kipaumbele pengine leo hii tusingekuwa tunashiriki katika mradi huu. Tunatambua na kuthamini mchango wenu kufanikisha ushiriki wa watanzania katika mradi. Vile vile, nitumie nafasi hii kuwahakikishia kuwa watanzania tulioaminiwa katika mradi huu tumeendelea kutekeleza kazi kwa ufanisi mkubwa na hatujawaangusha”, alieleza Bw. Wandiba.

Akizungumza katika ziara hiyo ya ukaguzi, Afisa anayeshughulikia masuala ya ushiriki wa watanzania kutoka PURA Bw. Ebeneza Mollel ameeleza kuwa PURA inajivunia kuona hatua ilizozichukua kuhakikisha watanzania wanapewa kipaumbele zimezaa matunda.

“Mwanzoni wakati mradi unaanza ushiriki wa watanzania kupitia ajira ulikuwa chini ya asilimia 20. Lakini hadi tunavyozungumza, ushiriki umeongezeka hadi kufikia asilimia 55. Mbali na ongezeko hilo, awali hapakuwa na mtanzania hata mmoja anayefanya kazi katika nafasi kama vile assistant driller na derrickmen lakini sasa tunaona watanzania wameaminiwa katika nafasi hizo. PURA pia imefanikiwa kuhakikisha kazi zisizohitaji ujuzi katika mradi huo zinafanywa na watanzania pekee” alibainisha Bw. Mollel.

Mradi wa ukarabati wa visima vya uzalishaji wa gesi asilia Songo Songo unatekelezwa na Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania LTD kupitia kampuni ya uchimbaji ya Exalo. Mradi huu ulianza kutekelezwa rasmi mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari, 2022. Mradi unalenga kukarabati visima vitatu ambavyo ni Songo Songo 3, Songo Songo 4 na Songo Songo 10 kwa lengo la kurejesha katika hali ya kawaida uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika visima hivyo.

Previous articleTMA YATOA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA KUANZIA MWEZI MACHI HADI MEI 2022
Next articleBoT: VIJANA WA KITANZANIA WAMEFAIDIKA NA MIFUKO YA UDHAMINI WA ELIMU YA MWALIMU NYERERE NA GILMAN RUTIHINDA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here