Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde ametoa mwito kwa wadau mbalimbali wa kilimo kutumia fursa ya uwepo wa Bima ya Mazao inayotolewa na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ili kuweza kupata usalama wa mazao yao kwa kunufaika na Bima hiyo pale wanapopata majanga.
Naibu Waziri Mavunde ametoa mwito huo leo Agosti 2,2022 alipotembelea Banda la NIC katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya ambapo alipata fursa ya kufahamu shughuli mbalimbali za Bima zinazofanywa na Shirika hilo ikiwemo Bima ya mazao.
Aidha amesema kuwa Shirika hilo linafanya kaza kubwa na nzuri ambapo amelishauri Shirika hilo kuwafikia wadau hao katika maeneo yao wakiwemo wakulima ili kuweza kutoa elimu na kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza wigo wa wakulima kujiandikisha katika Bima hiyo.
“Kikubwa ni Elimu na kuhakikisha wanawafikia wakulima katika maeneo yao juu ya manufaa ya Bima na kutoa fursa ya kukutana nao moja kwa moja na kujua mahitaji yao ili waweze kuyafanyia kazi na kuweza kuja na Huduma bora kwaajili ya wakulima hapa nchini” amesema Mhe.Mavunde.
Aidha ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo wamekuwa ikitoa msisitizo kwa wadau wote kuhakikisha kuwa wakulima wanatumia Bima kama sehemu ya kujikinga na majanga mbalimbali endapo yatatokea.
Sahirika la Bima la Taifa (NIC) limeweka kambi katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale ambapo wamekuwa wakikutana na wadau mbalimbali wanaotembelea maonesho hayo.