Home LOCAL GEITA MSINIANGUSHE, MSIIANGUSHE CCM – DKT. BITEKO

GEITA MSINIANGUSHE, MSIIANGUSHE CCM – DKT. BITEKO

*Awahimiza Wananchi Kupiga Kura Kesho, Kuchagua CCM*

* Awapongeza kwa Kampeni za Zakistaarabu*

* Ataka Siasa Ziwe Daraja la Kuunganisha na Kushindanisha Mawazo*

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wa Geita kujitokeza wa wingi kesho na kuchagua wagombea wa CCM.

Amewahimiza wananchi hao kuendelea kumuunga mkono yeye na CCM ili kutoa fursa ya kuendeleza jitihada za maendeleo “Nimekuja hapa kuwaambia msiniangushe wala kuiangusha CCM kwa kuwa miradi na juhudi zote zinazoendelea zinalenga kuleta maendeleo kwenu,”

Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 26, 2024 wakati akifunga Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Geita zilizofanyika katika Uwanja wa Mwenge, Uyovu, wilayani Bukombe.

Ameongeza kuwa kampeni za 2024 zimekuwa za kistaarabu huku akiwashukuru wanachama wa CCM kwa kuendeleza kauli mbiu ya Rais Samia ya kujenga Taifa moja la kuheshimiana na kustahimiliana.

Dkt. Biteko amebainisha sababu za kuwaomba wananchi hao kuipigia kura CCM kuwa “Wana Uyovu nataka niwakumbushe kazi ambazo zimefanywa tangu mwaka 2015, Kata hii ya Uyovu ilikuwa na shule za msingi tano, tumejenga saba sasa zipo 12, zilikuwa shule za sekondari mbili, tunajenga zingine ili ziwe sita,”

Ameendelea kusema Serikali inayoongozwa na CCM imeimarisha miradi ya maji, imejenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.2 na pia katika Wilaya ya Bukombe kitajengwa Chuo cha VETA.

Dkt. Biteko amesema kuwa na vyama vya upinzani si vibaya, watu washindane kwa hoja na sio kubaguana huku akiwataka wagombea wa CCM watakapochaguliwa wafanyekazi kwa uaminifu na uwazi ili kuchochea maendeleo.

“ Tunataka uchaguzi huu uwe wa amani, wa kistaarabu na wa haki kusiwe na kubebwa, uchaguzi huu usitufanye tugawanyike, ufanyike kwa amani na utufanye tuwe wamoja na baada ya uchaguzi tuijenge wilaya yetu, siasa ziwe daraja la kutuunganisha na kushindanisha mawazo,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Nicholous Kasandamila na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Alexandrina Katambi kwa nyakati tofauti wamewataka wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kesho na kuchagua wagombea wa CCM.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja amewashukuru wananchi wa Geita kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa ufungaji kampeni.

Pamoja na hayo Dkt. Biteko alishiriki Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizofanyika katika Wilaya tano za Mkoa wa Geita ambazo ni Mbogwe, Chato, Geita, Bukombe na Nyang’hwale.

Aidha, mkutano huo wa ufungaji kampeni umeambatana na burudani kutoka katika vikundi vya sanaa zaidi ya 40 pamoja na msanii mkubwa kutoka Kanda ya Ziwa, Magambo Machimu Lenga.

Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizinduliwa tarehe 20 Novemba, 2024 kwa Viongozi mbalimbali wa CCM kufanya uzinduzi katika mikoa mbalimbali ambapo Dkt. Biteko alizindua Kampeni hizo kwa Mkoa wa Mara.

http://GEITA MSINIANGUSHE, MSIIANGUSHE CCM – DKT. BITEKO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here