Home LOCAL TRAMPA YAZINDUA MAFUNZO MAALUMU KUWAJENGEA UWEZO WATAALAMU WA NYARAKA NA KUMBUKUMBU TANZANIA

TRAMPA YAZINDUA MAFUNZO MAALUMU KUWAJENGEA UWEZO WATAALAMU WA NYARAKA NA KUMBUKUMBU TANZANIA

Dar-es-Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) Devotha G. Mrope amezindua mafunzo maalumu yanayolenga kujenga uwezo wa kitaaluma kwa wataalamu wa taaluma ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini.
Bi. Devotha ameyasema hayo Aprili 8, 2024 katika Mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mafunzo haya yanalenga kuwawezesha watumishi wa umma na taasisi binafsi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na uadirifu katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.
“Mafunzo haya yatawakilisha juhudi za TRAMPA katika kujenga uwezo na kuimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini Tanzania. 
 
” Tunajitahidi kuhakikisha kuwa wataalamu wetu wanapata mafunzo na maarifa yanayohitajika ili kuhakikisha kuwa taarifa na nyaraka zinatunzwa kwa weledi na uadilifu,”  amesema  Bi. Devota.
Aidha, mafunzo hayo yamepangwa kufanyika Mei 6 hadi 9, 2024 mkoani Iringa katika ukumbi wa Masiti Grand Hall, na yanatarajiwa kuhudhuriwa na wataalamu wa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kutoka Tanzania bara na visiwani.
Mwenyekiti wa Chama hicho amesema kuwa hii ni fursa kwa washiriki kujifunza mbinu mpya na  bora za utunzaji wa kumbukumbu, uadilifu katika utunzaji wa siri za ofisi, na njia za kisasa za usimamizi wa nyaraka za taasisi.
Pia, kwa kuzingatia thamani ya mafunzo hayo, washiriki watalazimika kulipia gharama ya ushiriki ambayo ni shilingi laki nne tu (400,000), ambayo itagharamia uendeshaji wa mafunzo kwa muda wa siku nne.
Sambamba na hilo, Bi Devotha ametoa wito kwa waajiri kuwawezesha watumishi wao kuhudhuria mafunzo haya na kuwalipia stahiki zao.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wanataaluma
kuthibitisha ushiriki wao mapema ili kurahisisha maandalizi ya mafunzo hayo muhimu ambayo yatawezesha kuboresha utendaji na ufanisi katika utunzaji wa taarifa za umma na za binafsi.
“kada hii ni miongoni mwa kada zinazoongozwa na mifumo mingi, sambamba na miongozo kulingana na wakati. Hivyo, inalazimu wataalamu wajengewe uwezo kuendana na mazingira ya wakati husika” amesisitiza Bi. Devotha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here