Home BUSINESS KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YATEMBELEA MGODI WA BARRICK NORTH...

KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YATEMBELEA MGODI WA BARRICK NORTH MARA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo David, akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika mgodi wa Barrick North Mara (kushoto) ni Naibu Waziri wa Madini,Mh.Stephen Kiruswa na (kulia) ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda.
Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea Mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo wilayani Tarime na kutoa ushauri wa kuboresha sekta ya madini ili iweze kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla. Pia ilipongeza kampuni hiyo kwa kufanya uwekezaji mkubwa wenye tija na ufanikishaji wa miradi ya kijamii kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) sambamba na kuendeleza mahusiano na wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayozunguka mgodi.
Ziara ya Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Mh. David Mathayo David. Awali wajumbe wa Kamati hiyo walipata maelezo kuhusu shughuli za uendeshaji wa mgodi huo kabla ya kutembelea sehemu mbalimbali, ikiwemo eneo la majitaka, kinu cha kuchenjua dhahabu na baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa kutokana na fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) katika vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara.
Baadhi ya miradi hiyo ni Shule ya sekondari Matongo, mradi mkubwa wa maji wa Nyangoto na ule wa kilimo biashara unaoendeshwa na vijana katika kijiji cha Matongo.
Akiongea kwa niaba ya kamati baada ya kumaliza ziara hiyo, Dk.David Mathayo alisema “Kwa muda mfupi mmebadilisha mazingira ya mgodi huu. Mnatunza mazingira vizuri, wabunge wamefurahi – na kwa niaba yao ninawapongeza, endeleeni kuwa watunzaji wazuri wa mazingira kwa usalama wa wananchi wetu.”
Pia Kamati hiyo iliipongeza Barrick kwa kuendelea kuwa mfano mzuri katika ulipaji wa kodi mbalimbali serikalini, pamoja na utoaji wa mabilioni ya fedha za kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
“Kwenye kampuni kubwa za kibiashara ninyi [Barrick] mnaongoza kwa kulipa kodi na kutoa gawio kwa Serikali,” Mathayoalisema katika sehemu ya hotuba yake ya kuhitimisha ziara hiyo.
Kamati hiyo pia ilieleza kuridhishwa na jinsi Kampuni ya Barrick Gold inavyotekeleza Sheria ya ‘Local Content’ na hivyo kuwezesha Watanzania wengi wakiwemo wazawa wanaoishi jirani na migodi yake kunufaika na uwekezaji wake kupitia biashara na ajira, miongoni mwa mambo mengine.
Nao baadhi ya Wabunge wa kamati hiyo walipongeza Barrick kwa kuendelea kuleta mapinduzi kupitia uwekezaji mkubwa wa sekta ya madini nchini na walishauri mgodi uangalie uwezekano wa kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wajikwamue kiuchumi kwa kuwapatia baadhi ya maeneo wachimbaji hao.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Mh.steven Kiruswa ,alitoa wito kwa wadau waliopo kwenye sekta ya madini kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali ikiwemo kanuni inayohusiana na mgawanyo wa fedha za Uwajibikaji kwa jamii (CSR) na ushirikishwaji wa wazawa wa Tanzania katika shughuli za Mnyororo wa madini (Local content).
‘’Pamoja na changamoto tulizozisikia kutoka kwa viongozi wa wananchi wa eneo hili linalozunguka mgodi, natoa pongezi kwa kampuni ya Barrick kwa uendeshaji migodi yake nchini kwa weredi, uwazi na kuchangia pato la Taifa kupitia kodi, sambamba na kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido (katikati) akitoa ufafanuzi katika kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea mgodi wa Barrick North Mara ,(kushoto) ni Meneja wa mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko,(kulia) ni Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa mgodi huo Francis Uhandi.
Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido, aliwashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kutembelea mgodi huo na kuahidi kuwa maoni na ushauri uliotolewa na wajumbe yatafanyiwa kazi “Barrick siku zote tutahakikisha tunaendesha shughuli zetu kwa uwazi na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali”,alisisitiza.
Awali akitoa maelezo kuhusiana na shughuli za kampuni, Melkiory Ngido ,alisema Barrick kupitia migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu imewekeza hapa Tanzania shilingi zaidi ya trilioni sita, na kwamba kati ya kiasi hicho, Serikali imepokea trilioni tatu ambazo zimelipwa kwa mifumo wa kodi na gawio tangu mwaka 2019 ilipokabidhiwa na kuanza kuendesha migodi hiyo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Kuhusu mgodi wa North Mara, Ngido alisema: “Huu mgodi ulitakiwa kuisha [kufika kikomo] mwaka 2026 lakini kwa juhudi za uwekezaji na za kitaalamu utaenda hadi miaka 15 ijayo – utafika hadi mwaka 2039.”
Ngido, alisema Barrick kupitia mpango wake ujulikanao kama The Barrick-Twiga Future Forward Education Programme, imetoa Dola za Kimarekani milioni 30 sawa na shilingi takriban bilioni 70 kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari za juu upande wa mabweni na madawati, miongoni mwa mambo mengine katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mradi huu upo chini ya TAMISEMI na sisi kama Twiga na Barrick tunafurahi kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ili watoto wote waende A level (high school) na wasome katika mazingira rafiki,” alisema, Ngido.
Kamati hiyo ya Bunge pia ilielezwa kuwa asilimia 96 ya wafanyakazi takriban 3,000 wa Mgodi wa North Mara ni Watanzania, na kwamba juhudi za kuongeza idadi ya wafanyakazi wanawake zinaendelea.
Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeiagiza Serikali ya mkoa kumaliza tatizo la uvamizi katika mgodi wa North Mara unaofanywa na makundi ya watu (intruders) mara kwa mara kwa lengo la kuiba mawe yenye dhahabu.
“Uwekezaji huu ulindwe, hivi mpaka watu wanabeba mapanga na kuvamia mgodi, vyombo vyetu [vya ulinzi na usalama] vinakuwa wapi, vyombo visaidie kutatua tatizo hili (uvamizi mgodini) kwa sababu tunajirudisha nyuma wenyewe na tunaharibu taswira ya nchi yetu kwa wawekezaji,” alionya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mathayo.
Kwa upande mwingine, Kamati hiyo imeagiza Serikali ngazi ya wilaya na mkoa kumaliza malalamiko ya wananchi kuhusu mchakato unaotumika katika uthaminishaji wa ardhi inayohitajika kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za mgodi wa North Mara.
Baadhi ya viongozi waliofuatana na Kamati hiyo katika ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Madiwani na Wenyeviti wa vijiji kutoka Kata tano zenye vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi wa Noth Mara.
Migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu inaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiangalia utunzaji wa mazingira walipofanya ziara ya kikazi katika mgodi wa Barrick North Mara jana.
Baadhi ya wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakifuatilia maelezo kutoka kwa watendaji wa Barrick wakati walipotembelea mgodi wa North Mara
Diwani wa kata ya Nyamwaka, Mwita Marwa Magige akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika mgodi wa Barrick North Mara
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakikagua mradi wa kilimo biashara ulioanzishwa na mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo katika kijiji cha Matongo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here