Home LOCAL SERIKALI YACHUKUA HATUA ZA AWALI KUKABILI MAAFA HANANG’ MANYARA

SERIKALI YACHUKUA HATUA ZA AWALI KUKABILI MAAFA HANANG’ MANYARA


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga akiongoza timu ya uratibu wa masuala ya maafa kutoka Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa walipofika kujionea na kuchukua hatua za awali za kusaidia wakazi wa maeneo hayo walioathiriwa na maafa ya Maporomoko ya tope kutoka mlima Hanang’ mkoani Manyara.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa wakikagua maeneo yaliyoathiriwa na Maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang’ kijiji cha Gendabi Kata ya Gendabi Wilaya ya Hanang’ yaliyotokea tarehe 03 Disemba, 2023 mkoani Manyara.Ziara ilihusisha timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, kikosi kutoka kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa Pamoja na sekta zinazohusika ikiwemo TANROADS, TANESCO.

Mbunge wa Hanang’ Mhe. Samwel Hayuma akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Gendabi walioathiriwa na maafa ya maporomoko ya tope kutoka mlima Hanang.

Muonekano wa baadhi ya maeneo, nyumba na miundombinu iliyoharibiwa na maporomoko ya tope kutoka mlima Hanang’ mkoani Manyara, iliyotokea kufuatiwa mvua katika eneo hilo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU

NA. MWANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imechukua hatua za haraka kwa wahanga wa maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya tope yaliyotokea tarehe 03 Disemba, 2023 ambapo yalitoka mlima Hanang uliopo Mkoa wa Manyara na kusababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali yakiwemo mashamba, na makazi ya wananchi wa eneo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamefika katika kijiji cha Gendabi kata ya Gendabi Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara eneo yalipotokea maporomoko ya tope Leo tarehe 04 Disemba 2023.

Viongozi hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa Manyara Mhe. Queen Sendiga kufika katika Kijiji cha Gendabi ambalo ni eneo liliothirika Maporomoko ya tope kutoka Mlima wa Hanang yaliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 03 Disemba 2023.

Akiwa eneo la tukio hilo, Waziri Mhagama, amewaomba wananchi hao kupokea pole ambazo zinatoka kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambaye aliagiza lazima KUfika eneo la tukio na kuona nini kifanyike kwa dharura kuhusu uokoaji pamoja na makazi kwa waathirika hao.

“Mambo haya yakitokea kuna mambo ya haraka yanatakiwa yafanyike kwa dharura hivyo tumekuja na kushauriana namna ya kujipanga kwa pamoja ili kufanikisha jambo hilo kwa uharaka”. Ameongeza Mhagama.

Ameongeza kuwa, maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwanza kuona namna gani wanaweza kuendelea kuokoa watu na kazi hiyo wanaendelea nayo vikosi vya uokoaji, pia kuangalia namna gani ya kuweza kuwasitiri wenzetu waliotangulia mbele ya haki.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeshaleta wataalamu wa Miamba watatoa taarifa ya nini kilichotokea na nini kifanyike katika mlima wa Hanang.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kazi ya kufungua miundombinu ya barabara inaendelea ili kurahisia kazi za uokoaji na kufikisha huduma muhimu za kijamii katika meneo yaliyoathirika.

Amesema Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) tayari wamefungua Barabara ya Singida-Babati ambayo awali ilikuwa haipitiki kutokana na kujaa tope na magogo ya miti kutoka milimani.

Naye Mbunge wa Hanang’ Mhe. Samwel Hayuma aliipongeza serikali kwa namna inavyoendelea kuchukua hatua za haraka za kuokoa na kusaidia wahanga wa maafa hayo, huku akiwasisitiza wananchi hao kuendelea kuchukua tahadhari kwa maeneo yote yaliyoathirika na tope hilo.

MWISHO.

Previous articleWAZIRI MKUU AWASILI KATESH, ATOA POLE, AENDA KUKAGUA ENEO LA TUKIO
Next articleWAZIRI MKUU ATOA HESHIMA ZA MWISHO KWA WALIOFARIKI KATESH
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here