Home LOCAL ASA YAPONGEZWA UPATIKANAJI WA MBEGU BORA ZA KILIMO

ASA YAPONGEZWA UPATIKANAJI WA MBEGU BORA ZA KILIMO

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Nderiananga akiwa katika Viewing Point Tower wakati wa ziara yake ya kikazi katika shamba la mbegu Kilimi linalotekelezwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kupitia Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu  (Sera, Bunge na Uratibu)  alipofanya ziara hiyo Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Na Mwandishi wetu- Tabora

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameupongeza Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kwa kukamilisha Awamu ya Kwanza ya Mradi wa miundombinu ya Umwagiliaji katika shamba la mbegu Kilimi lililopo Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Mhe. Ummy ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika shamba la mbegu Kilimi linalotekelezwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kupitia Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ambapo amesema Taasisi hiyo iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo imepiga hatua kwa utekelezaji wa vitendo kwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa na imara ya Umwagiliaji katika shamba hilo.

Mtendaji  Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Dkt. Sophia Kashenge (wa tatu kulia) akitoa maelezo kuhusu shamba la mbegu za kilimo Kilimi kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga ( wa nne kushoto) wakati wa ziara yake mkoani Tabora

Amesema matarajio ya Serikali ni kuona uzalishaji wa mbegu unaongezeka kwa wananchi ili kupunguza uagizwaji wa mbegu kutoka Nchi jirani ambapo baadhi ya wakulima hushindwa kumudu gharama.

“Namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha tufanya kilimo cha kisasa na kupata fedha za kuendeleza sekta hii muhimu lengo la ziara hii ni kuona Mradi unavyoendelea hivyo nampongeza Waziri wa Kilimo Mhe. Bashe anafanya kazi kubwa sana akishirikiana na ASA. Pia nimefurahi kuona fedha inayokuja katika mradi inafanya kazi iliyokusudiwa kuongeza tija katika uzalishaji wa mbegu,”Alisema Mhe. Ummy.

Ameeleza kwamba Wizara ya Kilimo imejipambanua kwa kuweka miundombinu ya Umwagiliaji, kuhamasisha vijana kukipenda kilimo tofauti na awali kilichukuliwa kama adhabu.

“Tunawashauri watanzania waendelee kuiamini Serikali wakati tunafanya mapinduzi ya kilimo watumie fursa hii hasa waliopo katika maeneo haya na hata tutakapoanzisha vituo hivi katika maneno mengine basi wakulima watumie fursa hiyo kuboresha kilimo  wajikwamue kiuchumi,”Ameeleza.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Dkt. Sophia Kashenge amesema maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa mbegu ili kukidhi mahitaji ya wakulima hapa Nchini huku akisema kuwa wataendelea kuweka mikakati ya kuimairisha usalama katika mashamba kuepuka uharibifu unaotokana na uingizwaji wa mifugo katika mashamba hayo.

“Awali kulikuwa na changamoto kubwa ya mifugo kuingia katika mashamba lakini tumejitajidi kutoa elimu kwa vijiji vilivyopo katika maeneo haya na tunaendelea kuongeza ulinzi kimsingi mifugo ina madhara makubwa kwa mashamba ya mbegu na uzalishaji wa chakula pale mifugo inapoleta magugu kupitia kinyesi, wanaharibu rutuba ya udongo, kuongezeka kwa magonjwa kwa mazao hali inayoongeza gharama za matunzo,” Alifafanua Dkt. Sophia.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Nderiananga akikagua mifumo ya maji inayosambaza maji katika shamba la mbegu Kilimi linalotekelezwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kupitia Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu  (Sera, Bunge na Uratibu)  alipofanya ziara hiyo Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Naye Katibu Tawala Wilaya ya Nzega Bi. Winfrida Funto amemshukuru Mhe. Ummy kwa kufanya ziara katika Mkoa huo ambayo imetoa hamasa katika sekta ya kilimo hususan kilimo cha umwagiliaji ambacho hongeza tija kwa wakulima na kuondokana na kilimo cha mazoea.

Aidha mmoja wa wakazi katika Kijiji cha Bukamba Mpya Bi. Joyce Masanja ameishukuru  Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuratibu Mradi wa AFDP ambao kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) imewasaidia wakulima kupata mbegu bora za asili kutokana na uwepo wa mashamba ya uzalishi wa mbegu na kupatikana kwa urahisi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here