Na. Halfan Abdulkadir, ZANZIBAR.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Visiwani Zanzibar kimejigamba kushinda Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuendelea kuwaongoza Wazanzibari kutokana na kazi kubwa inayoendelea kufanyika chini ya Rais Dk Hussein Ali Mwinyi.
Kimeutaja ushindi huo wa CCM wa mwaka 2025 ni sawa na tetemeko lisilozuilika.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi na Uenezi, Khamis Mbetto Khamis ,wakati alipofungua kongamano la Wanawake Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mbetto aliwaeleza wanawake walioshiriki kongamano hilo akiwaahidi kuwa serikali ya CCM itaendelea kusimamia maslahi yote ya wanawake, kupinga ubaguzi wa kijinsia na aina yoyote ya ukatili dhidi yao .
Alisema Wanawake wa CCM ni jeshi lenye mtaji wa ushindi hivyo hayupo atakayewapuuza katika harakati za kuelekekea maendeleo ya kweli ya Zanzibar na watu wake.
“Wanawake mtabaki kuwa ni sehemu ya maendeleo, hayupo anayeweza kuwaweka benchi na kuwasahau . Kila mwanamke anathamani CCM tofauti na wale walioko upinzani .Nje ya CCM wanawake hubaguliwi Wala kutengwa” Alisema Mbetto.
Aidha Katibu huyo Mwenezi aliwanyooshea upande wa upinzani na kuutaka ufute ndoto za kushinda uchaguzi mkuu mwaka 2025 Kisiwani humo .
‘Iwapo mwanasiasa kigogo Maalim Seif Sharif Hamad hakushinda waliobaki ni maharage ya mbeya.” Alisema kwa kujigamba.
Mbetto alidai yuko Mwanasiasa mmoja wa upiinzani (hakumtaja jina) amedai mwaka 2025 chama chao kisipotangazwa kimeshinda Uchaguzi ujao, Zanzibar haitakalika na kumjibu kwa kusema hawezi kufanya lolote na kuwataka Wananchi kuwa na amani kufanya mambo yao ya maendeleo.
Mkoa wa Kaskazini Pemba ni miongoni mwa maeneo yanayoaminika kuwa ni ngome ya Upinzani ambapo mara kadhaa imekuwa ikishuhudiwa mchuano mkali wa Kisiasa ndani ya Mkoa huo Kila ifikapo Uchaguzi.