Home BUSINESS BRELA YAAGIZWA KUSHIRIKIANA KATIKA KUWEZESHA WAFANYABIASHARA

BRELA YAAGIZWA KUSHIRIKIANA KATIKA KUWEZESHA WAFANYABIASHARA

Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bi. Loy Mhando (kushoto), akimkabidhi cheti cha Usajili wa Jina la Biashara Eng. Naziru Kyaruzi baada ya kukidhi vigezo vya kusajili Jina la Biashara katika banda la BRELA lililopo katika Maonesho ya Sita (6) ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini 2023, Mjini Geita.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe(Mb), akihitimisha kongamano la Siku ya watoa huduma/ Leseni zinazohusiana na uchimbaji madini na Uwezeshaji Mitaji lililojumuisha Taasisi wezeshi , wajasiriamali na wachimbaji wadogo lililofanyika katika Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini 2023, yanayofanyika Mjini Geita, katika viwanja vya bombamili Mkoani Geita. Ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na taasisi wezeshi kutoa elimu kwa wananchi juu ya uwepo wa dirisha la pamoja lililoanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kupata huduma zote pamoja, badala ya kuwasumbua.

Afisa Leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Jubilate Muro akitoa mada juu ya umuhimu wa kupata Leseni ya Biashara kundi “A” katika Kongamano Maalum la Siku ya Watoa Huduma/Leseni zinazohusiana na Uchumbaji Madini na Uwezeshaji Mitaji, lililofanyika tarehe 22 Septemba, 2023 katika Maonesho ya Sita (6) ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini 2023 yanayofanyika mkoani Geita.

GEITA

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe(Mb), ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara (BRELA), na taasisi wezeshi kutoa elimu kwa wananchi juu ya uwepo wa dirisha la pamoja lililoanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kupata huduma zote pamoja na kuondoa usumbufu.

Mhe. Kigahe ametoa wito huo tarehe 22 Septemba, 2023 katika Kongamano Maalumu la siku ya watoa huduma na leseni zinazohusiana na uchimbaji madini na uwezeshaji mitaji lililojumuisha taasisi wezeshi na wajasiriamali pamoja na wachimbaji wadogo, katika Maonesho ya Sita (6) ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini 2023, yanayofanyika mjini Geita katika viwanja vya Bombambili Mkoani Geita.

“BRELA na taasisi nyingine, bahati nzuri sasa tuna dirisha la pamoja(Single Electronic Window System ) ambalo linawezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali ambazo zinahusika katika kupata Leseni, ambalo linamsaidia mafanyabiashara kupata Tax clearance , Namba ya Mlipakodi.”, alifafanua na kuongeza kuwa
“hii itasaidia kuondoa Kituo Jumuishi ( One Stop Centre ) ambacho kinamtaka mtu kuhangaika kwenda kwenye ofisi kuomba kibali, leseni na huduma nyingine. Hivyo tuwasaidie wananchi kupata huduma wanayohitaji papo kwa papo, “ameeleza Mhe. Kigahe

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bi. Loy Mhando ameeleza kuwa, agizo la Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara limepokelewa na kuahidi kulitekeleza kwa kuwa BRELA imekuwa ikiwafuata wananchi mahali walipo na kutoa huduma papo kwa papo.

“Jukumu la BRELA katika maonesho haya ni kutoa elimu ya urasimishaji biashara nchini, kutoa huduma za Usajili wa Majina ya Biashara na Huduma, utoaji wa Leseni papo kwa papo, sambamba na huduma za baada ya usajili”, amesema Bi. Mhando.

Aidha, ameongeza kuwa, BRELA katika maonesho haya, imejipanga kutoa huduma zote papo kwa papo ili kuwawezesha wafanyabiashara kukua na kutokuwa kikwazo kwao.

Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa hii ya manesho kurasimisha biashara na kampuni zote zilizosajiliwa kabla ya mfumo wa kielektroniki kuhuisha taarifa zao za Kampuni na Majina ya Bishara kuingizwa katika mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao(ORS).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here