Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka (kushoto), akizungumza na Meneja Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Vick Msina (katiakti), alipotembelea kwenye Banda la Benki hiyo, katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja John Mwakangale Jijini Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka (wa pili kulia), akizungumza na wanafunzi katika Banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alipotembelea kwenye banda la hilo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane, yanayofanyika kwenye viwanja John Mwakangale Jijini Mbeya. (kulia), ni Meneja Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania BoT Bi. Vick Msina.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
NA: HUGHES DUGILO, MBEYA
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka, amewataka watanzania kuwa na utaratibu wa kuwekeza, kwa kununua hati fungani Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kuwa Benki hiyo ni mahala salama kwa watanzania kuwekeza pesa zao, zitakazo wawezesha kufanya shughuli za kimaendeleo na kumudu gharama za maisha.
Mhe. Mtaka ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Agosti 5, 2023, alipotembelea Banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika Maonsho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane, yanayofanyika kwenye vya John Mwakangale Jijini Mbeya,
Amesema kuwa upo wajibu wa viongozi kuwahamasisha wananchi wote wakiwemo wafanyabiashara, wakulima na watuumishi katika Sekta zote za Umma na Binafsi, na kwamba, uwekezaji huo utawapa uwakika wa maisha yao baada ya kustaafu.
“Naamini kwamba tafsiri ya kustaafu inakuwa na maana zaidi kwa mtu ambaye ana hati fungani na kuanza kujifunza kufanya biashara taratibu, kuliko mtu ambaye amestaafu ndio anakuja kujifunza kufanya biashara wakati kwenye maisha yake yote hakuifanya.
“Ukishakuwa na hati fungani, kile kidogo unachokibakiza unaweza ukafungua biashara ndogo ya kukusaidia kuwa na shughuli ya kufanya kwa sababu sasa hauendi Ofisini kama zamani, hivyo utatumia muda huo kufanya shughuli zako za hapa na pale, huku ukiwa na uhakika kwamba sehemu kubwa ya pesa yako ipo mahala salama.
“Benki kuu inatoa elimu kubwa sana ya biashara ya kununua hati fungani, hii ni biashara ambayo watu wengi hawaifahamu, ni moja ya eneo ambalo ningetamani sana kila mtanzania aipate. BoT ndio mahala sahihi na salama ambapo mstaafu ataweka pesa yake ambayo itasimama kama dhamana kwa kile ambacho anataka kukifanya. Ameeleza Mhe. Mtaka.
Amesema kuwa wastaafu wengi wamekuwa wakirudi nyuma kutokana na kufanya biashara ambayo hana uzoefu nayo na kujikuta anafilisika ndani ya muda mfupi.
“Sekta binafsi wakubwa na wadogo sasa ni wakati sahihi wa kununua hati fungani, tupunguze walimu wengi, washauri baada ya kupokea fedha za kustaafu” amesema Mhe. Mtaka.