Home BUSINESS TAASISI ZA FEDHA ZATAKIWA KUPUNGUZA GHARAMA ZA RIBA YA MIKOPO

TAASISI ZA FEDHA ZATAKIWA KUPUNGUZA GHARAMA ZA RIBA YA MIKOPO

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Sila (kulia aliyesimama), akishuhudia zoezi la utiaji saini kati ya TWCC na gIz uliofanyika katika Mkutano wa Jukwaa la Utayari na fursa lililoandaliwa na TWCC kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (giZ). Mkutano huo umefanyika leo Julai 28,2023 Jijini Dar es Salaam. (wa pili kushoto aliyekaa), ni Kiongozi wa Programu ya kukuza ujuzi na ajira (E4D) Tanzania, Bi. Kabongo Mbunyi, na (wa pili kulia), ni Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Bi. Mwajuma Hamza, na (wa kwanza kushoto aliyesimama), ni Meneja Mradi wa kusaidia wanawake Wajasiriamali (WE4A), Faustine Msanjira.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo (wa pili kulia), akipiga makofi mara baada ya kushuhudia zoezi la kutia saini mkataba kati ya TWCC na giZ katika hafla hiyo iliyofanyika leo Julai 28,2023 Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akizungumza na wajumbe wananchama wa TWCC (hawamo pichani) katika Mkutano huo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Arbert Chalamila.

Kiongozi wa Programu ya kukuza ujuzi na ajira (E4D) Tanzania, Bi. Kabongo Mbunyi, akizungumza katika mkutano huo namna mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Kijerumani la giZ ulivyoweza kutoa mwanga kwa wajasiriamali wanawake nchini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Silla akizungumza katika mkutano huo muda mfupi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Arbert Chalamila.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo (kulia), akifurahia jambo na Mwenyekiti wa TWCC, Bi. Mercy Silla (kushoto) katika mkutano huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo (kushoto), akiwa na Kiongozi wa Programu ya kukuza ujuzi na ajira (E4D) Tanzania, Bi. Kabongo Mbunyi, (katikati), wakifuatilia hotuba ya ukaribisho ya Mwenyekiti wa TWCC, Bi. Mercy Silla, (hayumo pichani), katika mkutano huo.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

DAR ES SALAAM

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo , amezitaka Taasiza kifedha nchini, yakiwemo Mabenki kuweka viwango stahiki vya Riba na gharama za mikopo, ili kutoa fursa kwa wanawake wajasiriamali kukopa na kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali.
 
Mpogolo ameyasema hayo katika Jukwaa la Utayari na fursa lililoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia mradi wake wa Employment and Skills for the Development in Afrika (E4D).

Amesema ni muhimu benki nchini kuwa na mikopo rafiki riba nafuu kwa wanawake kwa sababu ndio watu wenye uhakika wa kurejersha fedha hizo kuliko wanaume ambao mara nyingi wamekuwa ni shida.
 
“Niwasihi benki mbalimbali kupunguza riba ili iweze kuendana na kasi ya kina mama wanayokwenda nayo, kutokana na riba kuwa juu ndio maana wanawake wanapata shida na kukimbilia mikopo ya halmashauri ya asilimia 10 ambayo peke yake haiwezi kuwatosha,” amesema

Aidha amesema kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo wanawake wanazipitia katika masuala ya fursa, mitaji na masoko ambazo zinapaswa kutatuliwa ili kuliwezesha kundi hilo kufanya biashara kwa uhuru na kujiingizia kipato.
 
“Moja ya suluhisho la jambo hilo ni kutumia masoko mtandao, hii ni fursa ambayo ikitumiwa vizuri itawakomboa wanawake wengi kiuchumi, leo hii mjasiriamali unayefikiria kutengeneza batiki na umepanga kutumia milioni 10 tenga kiasi kingine kwa ajili ya soko mtandao ambalo ukilitumia vizuri itakusaidia kujitangaza na kuuza bidhaa zako,” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila amewataka wanawake kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kuingia katika masoko makubwa ya kimataifa ya biashara na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
 
Sila amesema kwa sasa fursa za kiuchumi ni nyingi na Serikali imekwisha weka mazingira wezeshi ya wanawake kujikwamua hivyo ni muhimu kwa kundi hilo kuungana kwa pamoja na kufanyakazi kwa ushirikiano.
 
“Tukiungana tutafanikiwa kwa haraka, kama kuna mtu amepata oda kubwa ya bidhaa mbalimbali ni muhimu kuungana na mwenzake kuweza kufanikisha hilo, tunayasema haya kwa sababu tunataka wanawake kutoka chini nao waweza kunyanyuka kwa pamoja na wenzao waliofanikiwa,” amesema
 
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza amesema kazi yao ni kuhakikisha kwamba wanawake wanapata fursa za kiuchumi, wanashiriki kuzalisha ajira, kukuza kipato na kuchangia pato la taifa.

“Ili kuendana na mabadiliko la tekonolojia tumezindua pia soko mtandao kwa ajili ya wanawake ambapo wataweza kutumia simu janja yake na kuingia google na kupakua app ambayo imeandikwa iSoko, ukajisajili na kuweka bidhaa zake huko na mtu yoyote aliyopo nchini na nchi zingine za Afrika ataona,” amesema 

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ-E4D), Kabongo Mbuyi amesema wameamua kufadhili jukwaa hilo na kushirikiana na TWCC kwa lengo la kuwawezesha wanawake wajasiriamali kujikwamua kiuchumi.

“Tumekuwa tukifadhili program mbalimbali za wanawake lakini tumevutiwa na TWCC kwa kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuwainua wanawake lengo likiwa wajikwamue kichumi na kukuza pato la taifa la Tanzania,” amesema

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here