Home LOCAL MAKAMU WA RAIS KATIKA MAKABIDHIANO YA VIFAA TIBA BUHIGWE

MAKAMU WA RAIS KATIKA MAKABIDHIANO YA VIFAA TIBA BUHIGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria kupokea vifaa tiba kwaajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) vilivyotolewa na Taasisi ya Doris Mollel pamoja na vifaa tiba vilivyotolewa na Tume ya Ushindani katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Tarehe 06 Julai 2023. (wengine katika picha ni Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye na Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi Doris Mollel)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel kuhusu vifaa tiba kwaajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) vilivyotolewa na taasisi hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Tarehe 06 Julai 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimkabidhi mtungi wa gesi mwakilishi wa Mama wajawazito kutoka Wilaya ya Buhigwe Bi.Angel Leonce kwa lengo la kuhamasisha nishati safi ya kupikia pamoja na kukabiliana na changamoto zinazowakumba wajawazito. Mitungi hiyo imetolewa wakati wa hafla ya kupokea vifaa tiba vilivyotolewa na Taasisi ya Doris Mollel pamoja na vifaa tiba vilivyotolewa na Tume ya Ushindani (FCC) katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Tarehe 06 Julai 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wajawazito kwa kusindikizwa na wenzi wao kuhakikisha wanahudhuria kliniki wakati wote wa ujauzito ili kuweza kutambua mapema magonjwa na kuepukana na hatari za kuzaliwa mtoto kabla ya wakati.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba kwaajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) vilivyotolewa na Taasisi ya Doris Mollel pamoja na vifaa tiba vilivyotolewa na Tume ya Ushindani (FCC) katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Pia amekemea tabia za ukatili hususani kuwapiga wanawake wajawazito kwani madhara yake ni makubwa katika kupatikana kwa mtoto.

Ametoa rai kwa viongozi wa dini, serikali na kisiasa kushirikiana katika kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya ukatili kwa wanawake wajawazito.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewaasa watanzania kuachana na tabia za kuwapa msongo wa mawazo wanawake wajawazito kwani ni moja ya sababu zinazopelekea changamoto za uzazi ikiwemo kujifungua mtoto kabla ya wakati (njiti).

Pia Makamu wa Rais ametoa rai kwa wadau mbalimbali nchini wakiwemo wanamuziki, wachezaji na hata waigizaji kuunga mkono jitihada za serikali katika kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).

Ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel ambayo imekuwa ikitekeleza shughuli zake kwa takriban miaka nane sasa katika kusaidia Serikali kutoa huduma kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati na pia kusaidia katika utoaji wa vifaa tiba vinavyotumika kuokoa maisha ya watoto hao.

Aidha ameipongeza taasisi hiyo kwa kushirikiana na Oryx Energies Tanzania kujikita katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa akina mama wajawazito kwa kuwa tafiti zinaonesha mama mjamzito anayetumia nishati chafu katika kipindi cha ujauzito anakuwa yuko hatarini kupata mtoto njiti.

Amesema mpango huo ni muhimu kuwa endelevu kwani utatusaidia katika suala zima la kudhibiti uharibifu wa mazingira, ambao huchangiwa kwa kukata miti hovyo kwa ajili ya matumizi ya nishati. Ametoa rai kwa wananchi wa Buhigwe na maeneo mbalimbali nchini kuungana kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Pia Makamu wa Rais ameishukuru Tume ya Ushindani (FCC) kwa kujitoa kuchangia huduma za afya ikiwemo utoaji wa dawa na vifaa tiba kwa Wana-Buhigwe kama sehemu ya kuchangia ustawi wa jamii ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha huduma za jamii hususan tiba kwa wazazi na watoto chini ya umri wa miaka mitano kama sehemu ya mkakati wa kupunguza vifo vya uzazi.

Makamu wa Rais ametoa wito wa kuongeza juhudi katika kuhamasisha, kukuza uelewa na kujenga uwezo wa jamii kuhusu lishe bora hususan kwa mama na mtoto. Amesema hilo ni jambo muhimu la kuzingatiwa ili kujenga afya njema ya akina mama wajawazito na hatimaye afya njema kwa watoto watakaozaliwa.

Dkt. Mpango amewapongeza mchezaji wa kimataifa Mbwana Samatta na Mwanamuziki wa kizazi kipya Ali Saleh Kiba maarufu kama Ali Kiba kwa kuanzisha taasisi yao na kucheza mechi za hisani ambazo zimekuwa moja ya nyenzo za kuchangia maendeleo hapa nchini ikiwemo kutoa vifaa tiba kwaajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi Doris Mollel amesema Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika jitihada za kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati pamoja na changamoto zinazopelekea kuzaliwa kwa watoto hao.

Pia amesema taasisi hiyo imeshiriki katika kutoa vifaa tiba hapa nchini pamoja na utungaji sera za kukabiliana na ongezeko la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Bi. Mollel ameongeza kwamba taasisi imeendelea na jitihada za kuhakikisha marekebisho ya sheria ya likizo yanafanyika ili kuwapa muda wa miezi sita wakina mama wanaojifungua watoto kabla ya wakati kutokana na changamoto zinazowakumba.

Pia amesema tayari taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wamefanikiwa kuhakikisha bima binafsi zinatoa huduma kwa mtoto anayezaliwa kabla ya wakati kupitia gharama ya bima ya mama wa mtoto.

Mwakilishi wa Tume ya Ushindani (FCC) Bi Monica Moshi ambao wametoa vifaa tiba kwa Wilaya ya Buhigwe amesema utoaji wa vifaa tiba katika halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ni sehemu ya kuchangia ustawi wa jamii jukumu ambalo wamekua wakitekeleza kila mwaka ikiwa ni hatua ya kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha huduma za tiba nchini hususani zile za uzazi na watoto chini ya miaka mitano ikienda sambamba na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Hafla hiyo pia imehusisha upokeaji wa Madawati 450 kutoka Shirika la Maendeleo la Uturuki TIKA pamoja na utoaji wa mitungi ya gesi 300 kwajili ya Mama wajawazito na wahudumu wa Afya.

Previous articleWAZIRI MKUU MAJALIWA AMEWATAKA WATANZANIA KUTUMIA KISWAHILI KUKUZA UCHUMI
Next articleWATAKWIMU NA WALIMU SKULI ZA MSINGI WATAKIWA KUJIFUNZA KWA BIDII
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here