Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwasha Mwenge wa Uhuru, wakati alipozindua Mbio za Mwenge huo kitaifa kwa mwaka 2023 katika uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Aprili Mosi , 2023. Katikati ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu Ofisi wa Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Jamali Katundu na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Kiongozi wa mbio hizo , Abdallah Shaib Kaim, wakati alipozindua Mbio za Mwenge huo Kitaifa kwa mwaka 2023, katika uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Mtwara wakati alipozindua Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 katika uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Aprili Mosi, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Azindua mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa 12 wachukue hatua stahiki kutatua tatizo la udumavu uliozidi wastani wa kitaifa kwenye mikoa yao na kuhimiza lishe bora.
“Mikoa yenye kiwango kikubwa cha udumavu zaidi ya wastani wa kitaifa ni pamoja na Iringa inayoongoza kwa asilimia 56.9, Njombe (asilimia 50.4), Rukwa (asilimia 49.8), Geita (asilimia 38.6) Ruvuma (asilimia 35.6), Kagera (asilimia 34.3), Simiyu (asilimia 33.2), Tabora (asilimia 33.1), Katavi (asilimia 32.2), Manyara (asilimia 32), Songwe (asilimia 31.9) na Mbeya (asilimia 31.5). Viongozi wa Mikoa hii waitafakari hali hii na kuchukua hatua stahiki,” amesema.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Aprili Mosi, 2023) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani waliofika kushuhudia uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona, katika Manispaa ya Mtwara.
“Taarifa zilizopo zinaonesha hali ya lishe miongoni mwa Watanzania hairidhishi kutokana na kuathiriwa na tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, uzito pungufu, ukondefu na uzito uliozidi pamoja na uliokithiri (kiribatumbo),” amesema.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema hali ya uzito uliozidi na uzito uliokithiri (kiribatumbo) ndicho kiashiria pekee ambacho hakijawahi kupungua na kimeendelea kuongezeka kutoka asilimia 11.3 mwaka 1991 hadi kufikia asilimia 31.7 mwaka 2018 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar uzito uliozidi umefikia asilimia 41.8 katika kipindi hichohicho.
Amesema tatizo la uzito uliozidi na kiribatumbo ni kubwa katika mikoa ya Kilimanjaro ambako wana asilimia 49, Dar es Salaam (asilimia 48.6), Mjini Magharibi (asilimia 47.4) na Kusini Unguja (asilimia 39.4). “Hali hii inaelekea kuwa janga la kitaifa na kisababishi kikubwa cha kuongezeka baadhi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani na magonjwa ya moyo.”
“Wananchi wenzangu, sasa ni wakati muafaka wa kubadili mitindo ya maisha yetu kwa kufanya mazoezi angalau nusu saa kila siku na kula mlo kamili sambamba na kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, pombe na sigara,” amesisitiza.
Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwenye mikoa yote 31 na Halmashauri 195 kwa siku 196. Waziri Mkuu aliuwasha mwenge huo saa 6.06 mchana na saa 6.07 akamkabidhi Kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Bw. Abdallah Shaib Kaim (anayetoka Kaskazini Pemba). Saa 6.08, Bw. Shaib alikiri kuupokea mwenge huo na kuahidi kuwa ataukabidhi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ifikapo Oktoba 14, mwaka huu ukiwa salama.
Wakimbiza mwenge wengine na mikoa wanayotoka ni Bw. Martin Michael Mkanga (Mtwara), Bi. Atupokile Elia Mhalile (Dodoma), Bi. Zainab Hemed Mbetu (Kusini Unguja), Bw. Emmanuel Jackson Hondi (Manyara) na Bw. Juma Silima Sheha (Kaskazini Unguja).
Kaulimbiu ya mwaka huu imelenga maeneo makuu sita yakiwemo ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira, mapambano dhidi ya rushwa, UKIMWI, dawa za kulevya, malaria na lishe bora. Ujumbe maalum wa mbio hizo ni: “Umuhimu wa kuhifadhi mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ni kuboresha huduma za kijamii na maisha ya Watanzania katika sekta za elimu, afya, maji na barabara. Hatua hizo, zinakwenda sambamba na uwekezaji mkubwa katika usafiri na usafirishaji nishati ya umeme, kilimo cha uhakika na viwanda.
“Hata hivyo, nyote mtakubaliana nami kwamba ufanisi wa huduma hizi kwa kiasi kikubwa unaathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira ambao kwa takribani asilimia 95 ni matokeo ya shughuli za kibinadamu.”
Amesema Tanzania ni moja ya nchi zinazoathiriwa na changamoto za uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya tabianchi kupitia shughuli zisizo endelevu za kibinadamu zikiwemo uvamizi wa maeneo tengefu, vyanzo vya maji na matumizi holela ya mbolea zenye kemikali na viuatilifu; ufugaji wa kuhamahama unaojumuisha makundi makubwa ya mifugo na ukataji holela wa miti kwa ajili ya kuni.
Shughuli nyingine ni uchomaji wa mkaa na upanuzi wa mashamba na makazi; uchomaji moto ovyo wa misitu na mbuga, uchimbaji wa madini usio endelevu na uvuvi haramu, uvunaji haramu wa mikoko na kuenea kwa viumbe vamizi.
Mbio za mwenge wa uhuru ziliasisiwa mwaka 1961 na Baba wa Taifa, Hayati Julius K. Nyerere ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika. Na umekuwa ukikimbizwa katika mikoa yote ili kuhamasisha amani, uzalendo, umoja na mshikamano.